Prime
Siku tatu za hesabu kali CAF
Muktasari:
- Kabla ya hapo ilifungwa ugenini 1-0 na Stellenbosch inayoongoza kundi C ikiwa na pointi nne. Ndiyo timu pekee katika kundi hilo haijaonja ladha ya kipigo katika mechi mbili za kwanza ikishinda na kupata sare.
Dar es Salaam. Wikendi hii, kuna mechi nne zinazochezwa ndani ya siku tatu kwa maana ya Ijumaa, Jumamosi na Jumapili zikiwa na hesabu kali kwa wawakilishi wa Tanzania wanaoshiriki mashindano ya kimataifa ngazi ya klabu.
Wawakilishi hao ni Yanga na Simba wanaoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam na Singida Black Stars wakiwa Kombe la Shirikisho.
Hesabu kali za wawakilishi hao zinakuja kufuatia matokeo ya mechi mbili za kwanza kabla ya michuano hiyo kusimama kupisha Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 zilizofikia tamati jana Jumapili ambapo wenyeji Morocco ilicheza na Senegal.
Al Ahly vs Yanga
Tukianza Ijumaa ya Januari 23, 2026, mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara na washindi wa Kombe la Mapinduzi 2026, Yanga, itakuwa Misri kucheza na Al Ahly katika mechi ya tatu kundi B itakayopigwa kwenye Uwanja wa Borg El Arab uliopo Alexandria kuanzia saa 12:00 jioni.
Matokeo ya mechi mbili za kwanza yanaifanya mechi hiyo kuwa ngumu kwani timu hizo zinalingana pointi zote zikiwa na nne baada ya kushinda moja na sare moja. Ndiyo timu pekee za kundi hilo hazijapoteza hadi sasa.
Al Ahly wameipeleka mechi hiyo huko ikiwa ni mwendo wa wastani wa saa nne kutoka Cairo kwa usafiri wa treni au basi.
Yanga si wageni wa uwanja huo kwani iliwahi kupelekwa na wapinzani wao hao mwaka 2016 na kupasuka mabao 2-1, ikatolewa katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya awali kutoka sare ya bao 1-1 Dar es Salaam na kushindwa kutinga makundi.
Uwanja huo umekuwa ukitumiwa na Al Ahly na wapinzani wao, Zamalek kwa ajili ya mechi zote ngumu wakiukimbia Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, jambo ambalo Yanga inapaswa kuanza kujiweka sawa kabla ya kuwafuata washindani wao hao wanaolingana nao pointi kwa sasa kundini.
Licha ya kuonekana ni mkakati maalumu kwa wenyeji kulipeleka pambano hilo Borg El Arab, lakini mabosi wa Yanga ni kama wameshtukia mapema kwa kuanza maandalizi ya kucheza huko wakitanguliza watu kuweka mambo sawa, wakisubiri kikosi kuondoka Jumatano.
Yanga itakuwa na saa zisizopungua 48 kabla ya kuvaana na Al Ahly inayoongoza msimamo kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa, ikiwa na matano na kufungwa mawili wakati Yanga imefunga moja tu ilipoichapa AS FAR Rabat kwa bao 1-0 Zanzibar.
Ahly msimu huu mechi zake za kimataifa zimekuwa zikichezwa kwenye Uwanja wa Al Salaam uliopo jijini Cairo unaochukua mashabiki 30,000, ambapo hapo walizipeleka JS Kabylie ya Algeria na kuifunga 4-1 kisha Aigle Noir hatua ya mtoano waliposhinda 1-0.
Mechi mbili za nyuma ambazo Yanga ilicheza dhidi ya Ahly ilitumia Uwanja wa Kimataifa wa Cairo unaochukua mashabiki 75,000 kwenye michezo iliyopigwa Machi Mosi, 2024 ikifungwa bao 1-0, kisha ule wa Machi 9,2016 ikipoteza kwa mabao 2-1.
Yanga imepanga kuondoka nchini alfajiri ya keshokutwa Jumatano ambapo ikitua Cairo moja kwa moja itawahi Alexandria kabla ya kukutana na Ahly Ijumaa ya Januari 23, 2026 kisha usiku huohuo itarejea Cairo baada ya mechi ili kurudi nchini tayari kwa pambano la marudiano dhidi ya Waarabu hao Januari 30, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Katika kundi hilo, JS Kabylie pia itaikaribisha AS FAR Rabat kwenye Uwanja wa Hocine Aït Ahmed uliopo Tizi Ouzou nchini Algeria. Timu hizi zina pointi moja zikiwa pia zimepoteza mechi ya kwanza dhidi ya wababe wa kundi hilo, Yanga na Al Ahly.
Kundi B
P W D L GF GA Pts
1. Al Ahly 2 1 1 0 5 2 4
2. Yanga 2 1 1 0 1 0 4
3. AS FAR 2 0 1 1 1 2 1
4. JS Kabylie 2 0 1 1 1 4 1
Espérance v Simba
Jumamosi Januari 24, 2026, Simba itakuwa ikiipigania bendera ya Tanzania huko nchini Misri itakapokaribishwa na wenyeji wake Espérance, mechi iliyopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Hammadi Agrebi uliopo mji wa Tunis kuanzia saa 11:00 jioni.
Simba ipo kwenye mtihani mkubwa zaidi inapokwenda kucheza dhidi ya Espérance kwani haina pointi ikiburuza mkia wa kundi D baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza dhidi ya Petro Atletico (1-0) na Stade Malien (2-1).
Wapinzani wao, Espérance, wana pointi mbili walizozipata mechi za kwanza nyumbani ilipotoka 0-0 dhidi ya Stade Malien na sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Petro Atletico.
Waarabu hao wanausaka ushindi wa kwanza huku Simba pia ikisaka pointi tatu za kwanza ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuifukuzia nafasi ya robo fainali iliyofuzu mara sita katika michuano ya CAF kuanzia mwaka 2018 hadi 2025.
Simba chini ya Kocha Steve Barker, inalazimishwa kushinda mechi hii na ile ya marudiano itakayochezwa kati ya Januari 30 na Februari 1, 2026 jijini Dar es Salaam kwani ikiteleza safari yake ya kufuzu robo fainali itakuwa na asilimia chache zaidi na itakuwa mara ya kwanza Simba kushindwa kufuzu hatua hiyo tangu icheze makundi ya CAF tangu 2018.
Wakati vibonde hao wa kundi wakipambana wenyewe, wababe nao wanakutana, Stade Malien itakuwa mwenyeji wa Petro Atletico. Mechi ikicheza Jumapili Januari 25, 2026. Timu hizo zina pointi nne, kila moja ikisaka ushindi kuongoza kundi. Baada ya hapo, zitarudiana kule nchini Angola, Petro Atletico ikiwa mwenyeji.
Kundi D
P W D L GF GA Pts
1. Petro Atletico 2 1 1 0 2 1 4
2. Stade Malien 2 1 1 0 2 1 4
3. Espérance 2 0 2 0 1 1 2
4. Simba 2 0 0 2 1 3 0
Nairobi United v Azam
Vijana wa Florent Ibenge, Azam FC, Jumapili ya Januari 25, 2026 watakuwa pale nchini Kenya kwenye Dimba la Nyayo lililopo jijini Nairobi kucheza dhidi ya wenyeji wao, Nairobi United.
Azam na Nairobi United hazina pointi katika kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza mechi zote mbili za kwanza, zinatofautiana tu mabao ya kufungwa, huku zote zikiwa hazijatikisa nyavu za wapinzani.
Azam iliyocheza dhidi ya AS Maniema na Wydad, imepoteza mechi zote hizo ikifungwa jumla ya mabao matatu, huku Nairobi United nayo ikipoteza dhidi ya timu hizo kwa jumla ya mabao manne.
Saa 10:00 jioni mechi hii imepangwa kuanza kuchezwa ambapo Azam itakuwa na wakati mzuri wa kutafuta pointi za kwanza, hata hivyo wapinzani wake nao hawapo kinyonge.
Timu hizi zote zinashiriki hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza, hivyo zinakutana zikiwa hazina uzoefu mkubwa. Kumbuka baada ya hapa, Azam itakuwa mwenyeji wa Nairobi United, Februari 1, 2026.
Kundi B
P W D L GF GA Pts
1. Wydad AC 2 2 0 0 4 0 6
2. AS Maniema 2 2 0 0 3 0 6
3. Azam 2 0 0 2 0 3 0
4. Nairobi Utd 2 0 0 2 0 4 0
Singida BS v AS Otohô
Pointi moja iliyoipata Singida Black Stars katika mechi iliyopita nyumbani dhidi ya Stellenbosch katika sare ya 1-1, imewapa nguvu ya kukaribisha AS Otohô kwenye Dimba la New Amaan Complex lililopo Zanzibar, Jumapili ijayo Januari 25, 2026 kuanzia saa 1:00 usiku.
AS Otohô kutoka Congo Brazzaville, ina pointi tatu ilizopata katika ushindi wa 4-1 dhidi ya CR Belouizdad nyumbani. Kabla ya hapo ilifungwa ugenini 1-0 na Stellenbosch inayoongoza kundi C ikiwa na pointi nne. Ndiyo timu pekee katika kundi hilo haijaonja ladha ya kipigo katika mechi mbili za kwanza ikishinda na kupata sare.
Faida ya Singida Black Stars kuelekea mechi hii, inarudi tena nyumbani huku ikiwa na maboresho ya benchi la ufundi ambapo sasa kocha mkuu ni David Ouma aliyechukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyepewa cheo cha mkurugenzi wa ufundi, huku Othmen Najjar akiajiriwa kuwa meneja mkuu wa timu. Ramadhan Nswanzurimo sasa ni mshauri wa ufundi. Wasaidizi wa Ouma wanaendelea kubaki kuwa Mousa Nd'aw na Muhibu Kanu.
Ili Singida itoke mkiani mwa kundi na kuendelee kuwa na matumaini ya kufuzu robo fainali, inapaswa kuichapa AS Otohô nyumbani, kisha ikienda ugenini isipoteze tena zitakaporudiana Februari 1, 2026.
Kundi C
P W D L GF GA Pts
1. Stellenbosch 2 1 1 0 2 1 4
2. AS Otohô 2 1 0 1 4 2 3
3. CR Belouizdad 2 1 0 1 3 4 3
4. Singida BS 2 0 1 1 1 3