Onyo la dawa za usingizi kwa nyota wa England Kombe la Dunia
Kikosi cha timu ya Taifa ya England kitakachoshiriki katika Fainali za Kombe la Dunia 2026. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Katika Fainali za Kombe la Dunia 2026, England imepangwa kundi L na timu za Panama, Croatia na Ghana.
Mtaalamu wa usingizi, James Wilson amewashauri wachezaji wa timu ya Taifa ya England kutotumia dawa za usingizi katika kipindi chote watakachokuwa katika fainali za Kombe la Dunia.
Wilson ambaye amewahi kufanya kazi katika klabu za Coventry City, West Ham United, Rotherham na Lincoln amesema kwamba kitaalam, matumizi ya dawa za usingizi hayamsaidii kumrejesha mchezaji katika hali ya kawaida ya mwili wake baada ya mchezo.
"Kutokana na mazungumzo niliyofanya na wachezaji, katika soka la wanaume na la wanawake, ninatumaini tu kwamba watu hawatumii dawa za usingizi.
“Dawa za usingizi hazikupi usingizi wa kuimarisha mwili na kusaidia kupona. Kile unachopata ni hali ya kutulizwa au kulegezwa mwili, na hukufanya ulale bila kujitambua.
“Kwa ujumla, dawa hizo si nzuri kwa usingizi wako wala kwa mchakato wa kupona kwa mwili, ndiyo maana si wazo zuri kuzitumia katika mpira wa miguu," amesema Wilson.
Wilson ameongeza, "kweli kwamba dawa hizo zinaweza kusababisha utegemezi (uraibu) ni sababu nyingine kubwa ya kuonyesha kwa nini hatupaswi kuzitumia, hasa kama njia ya kwanza ya kukabiliana na matatizo ya usingizi.
“Saa nne za usingizi usioridhisha katika usiku baada ya mechi bila kutumia dawa za usingizi ni bora kuliko saa nane za usingizi unaotokana na matumizi ya dawa nyingi za usingizi.”
Katika Fainali za Kombe la Dunia 2026, England imepangwa kundi L na timu za Panama, Croatia na Ghana.
Itaanza kwa kucheza na Croatia, Juni 17 na Juni 23 itakabiliana na Ghana na itamaliza hatua ya makundi kwa kuikabili Panama, Juni 28.