Osaka apania kuongoza kizazi kipya, amzimia Serena

Monday February 22 2021
Osaka pic

Bingwa wa michuano ya wazi ya Australia, Naomi Osaka amesema anajisikia vizuri kuwa kioo cha kizazi kipya baada ya taji la nne la Grand Slam kuimarisha nafasi yake katika mstari wa mbele wa enzi mpya ya mchezo wa tennis duniani.
Lakini nyota huyo wa kike wa Japan, ambaye ametwaa taji la nne la michuano mikubwa akiwa na miaka 23 tu, amesema Mmarekani Serena Williams, 39 -- ambaye ametwaa mataji 23 makubwa, anaendelea kuwa sura ya mchezo huo wa tennis duniani.
Osaka alimshinda Mmarekani Jennifer Brady kwa michezo 6-4, 6-3 katika fainali ya michuano ya wazi ya Australia Jumamosi na kutwaa taji hilo la nne kutoka katika mashindano nane aliyoshiriki, na kuendeleza ushindi wake mfululizo hadi mechi 21.
Anaingia katika orodha iliyo na Monica Seles na Roger Federer waliotwaa mataji manne makubwa ya kwanza, na atapanda hadi nafasi ya pili katika orodha ya ubora duniani.
Osaka alimuondoa Serena Williams katika nusu fainali baada ya kumshinda katika fainali kali ya michuano ya wazi ya Marekani (US Open) mwaka 2018 na kutwaa taji lake la kwanza kubwa.
Lakini alipoulizwa kama sasa anamuondoa Williams kutoka katika orodha ya wachezaji ambao ni taswira ya mchezo wa tennis kwa wanawake duniani, Osaka alijibu: "Hapana, hapana kabisa."
Alitumia maneno hayo matatu tu kujibu kuhusu Serena, akisema alitaka kuwa mkweli kuhusu mambo yake binafsi.
"Nimejifunza ndani na nje ya uwanja kutokuwa na uhakika kuhusu wewe mwenyewe," alisema.  
"Nina amani na hapa nilipo na kusema kweli ninafurahia kucheza mashindano ya Grand Slam katika kipindi janga (la corona)."
Baada ya kutwaa ubingwa wa pili wa michuano ya Australia, Osaka alitumia muda mwingi kutia saini ya kumbukumbu katika vitu vya watu, akiashiria kuwa alisifiwa sana katika mitandao ya kijamii.
Alisema bado anakua lakini anategemea kuwa hamasa kwa wachezaji chipukizi.

Advertisement