Pablo kuja na sapraizi Simba

Wednesday January 12 2022
PABLO PIC
By Mwanahiba Richard

UNGUJA. Alhamisi Januari 13 ni fainali kati ya Azam Fc na Simba itakayoanza saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani hapa huku kocha wa Simba Pablo Franco akisema wanakuja na sapraizi kwa mashabiki wao.

Hata hivyo Pablo hakusema itakuwa ni sapraizi ya aina gani huku akitamba kuwa wanatwaa ubingwa huo na wanaenda kubadilisha historia kwenye mashindano hayo ya Kombe la Mapinduzi.

Azam ndiyo timu pekee iliyotwaa ubingwa huo mara nyingi ikibeba mara tano huku Simba ikitwaa mara tatu.

Pablo amesema kuwa kila kitu kipo sawa na wanawaheshimu wapinzani wao kwani ni timu bora na wametoka kucheza nao hivi karibuni mechi.

"Mechi itakuwa ngumu kwasababu hata Azam ni bora ila mashabiki wetu watarajie mambo mazuri ambayo tunakuja nayo kwenye mechi hiyo. Kutwaa ubingwa ni moja ya malengo yetu na tumefikia sehemu nzuri kwa asilimia kubwa," amesema Pablo

Naye mchezaji wa timu hiyo Shomari Kapombe amesema wapo tayari na tunaamini tutashinda kwani tumejipanga vizuri.

Advertisement

"Tumetoka kucheza na Azam hivi karibuni na tuliwafunga hivyo hata sasa tumejipanga kushinda na kutwaa ubingwa huo ambao hatujabeba miaka mingi. Wanasimba tuna kiu ya ubingwa huu hivyo watarajie makubwa," amesema

Advertisement