Prime
Pacome, Aziz KI na Ahoua wampa mtihani Ecua
Muktasari:
- Ecua mwenye miaka 23, anatajwa kuwa mchezaji imara mwenye kasi, chenga na jicho la kuliona lango.
Dar es Salaam. Baada ya kujitangaza mwenyewe kupitia kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa sasa ni mchezaji wa halali wa Yanga Ecua Celestine anakuwa MVP wa tano kutoka Ligi Kuu ya Ivory Coast kutua Ligi Kuu Bara, huku watangulizi wake wakimpa ugumu.
Ecua juzi, alijitambulisha rasmi kuwa yenye ni mchezaji wa Yanga na kumaliza tetesi zilizokuwa zikizagaa muda mrefu kuwa amemalizana na timu hiyo, lakini jambo kubwa ni kwamba msimu uliomalizika ndiye alikuwa mchezaji bora wa ligi hiyo.
Staa huyo alimaliza msimu akiwa amefunga mabao 15 na kutoa pasi 12 za mabao, akiwa ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kwenye Ligi Kuu ya nchi humo msimu huu baada ya kuhusika kwenye mabao 27, mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita alikuwa Jean Charles Ahoua.
Kwa misimu mitano mfululizo kila mchezaji aliyekuwa MVP kwenye Ligi Kuu ya Ivory Coast, ametua nchini na kujiunga na timu mojawapo kubwa kati ya Simba, Yanga na Azam na tayari wanampa staa huyo deni kubwa.
Alianzia Kipre Junior msimu wa 2021/2022 ambaye alijiunga na Azam, akafuata Stephen Aziz Ki msimu wa 2022/2023 alijiunga na Yanga na baada yake akatua Pacome Zouazoa naye akajiunga na Yanga na mwisho alitua Jean Charles Ahoua kwenye kikosi cha Simba na sasa Ecua ambaye baada ya ligi kumalizika ndiye katangazwa kuwa mchezaji bora.
Hata hivyo, nyota ya Ecua atatakiwa kufanya mambo makubwa kutokana na kile ambacho watangulizi wake wameshafanya kwenye ligi kuu hadi sasa ambapo kila mmoja amekuwa akionyesha ubora wa hali ya juu na kila mmoja ameshaweka alama yake hadi sasa.
Kipre akiwa na Azam msimu wake wa pili ulikuwa bora ambapo alihusika na mabao 18 akiwa ndiye mchezaji mahiri zaidi kwenye timu hiyo kwa msimu huu na baada ya hapo alipata dili ambapo alijiunga na timu kubwa zaidi ya USM Alger .
Kwa upande wa Aziz Ki ambaye amejiunga na klabu kubwa ya Wydad Casablanca ya Morocco, alifanya vyema kwenye msimu wake wa pili tangu alipotua Yanga ambapo alifunga mabao 21 na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, huku Pacome akionyesha ubora wa juu kuanzia msimu wake wa kwanza na msimu uliopita alikuwa imara zaidi baada ya kuhusika kwenye mabao 22, akifunga 12 na kutoa pasi kumi za mabao.
Hata hivyo, Ahoua yeye amekuwa tofauti na watangulizi wake ambapo amefanikiwa kuwika kwenye msimu wake wa kwanza, akiwa na timu yake ambapo amemaliza msimu uliopita akiwa kinara wa mabao baada ya kufunga 16 na kutoa pasi tisa za mabao, hivyo kuhusika na mabao 25, mawili nyuma ya Ecua aliyeifanya ASEC kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya Ivory Coast.
Hii ina maana kuwa nyota huyo ambaye aliitumikia ASEC kwa mkopo akitokea kikosi cha Zoman FC ambacho kimemaliza msimu ikiwa nafasi ya kumi kwenye msimamo wa ligi atatakiwa kuhakikisha anawaridhisha mabosi wa Jangwani kwa kuwa mambo makubwa kama ambavyo wamefanya ma MVP wengine, jambo ambalo linaonekana kuwa analiweza.
Usajili wa Ecua ndani ya kikosi cha Yanga unatajwa kuwa moja ya hatua muhimu kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, na michuano ya kimataifa, ambapo msimu uliopita Yanga iliishia hatua ya makundi na sasa tageti yao ni kufika hapo hapo.
"Bado tageti yetu ni kufika hatua ya makundi, hatujabadilisha baada kufika hapo ndiyo tutaseti nyingine kwenda mbele zaidi na nataka kuwahakikishia kuwa itakuwa historia tukishatua makundi," alisema Rais wa Yanga Hersi Said.
Ecua mwenye miaka 23, anatajwa kuwa mchezaji imara mwenye kasi, chenga na jicho la kuliona lango. Anatarajiwa kuongeza ushindani kwenye safu ya ushambuliaji ya Wanajangwani, ambayo imekuwa ikiwategemea zaidi Prince Dube pamoja na Clement Mzize ambaye inaelezwa baada ya dili hili kukamilika anaweza kutimka kwenye timu hiyo, huku Zamalek ya Misri ikitajwa.
Huu unaonekana kuwa usajili sahihi kwenye timu hiyo baada ya msimu uliopita kuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri wa ASEC ambapo alifunga mabao mawili kwenye michezo minne aliyocheza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
WASIFU
Jina: Celestine Ecua
Umri: 23 (01.01.2002)
Uraia: Ivory Coast (Côte d'Ivoire)
Nafasi uwanjani: Mshambuliaji, Winga
Timu alizopita: ASEC Mimosas, Zoman FC, AS Denguelé