Picha lote Manyama, Simba, Azam

Saturday June 12 2021
manyaama pic
By Waandishi Wetu

HEBU kaa kwanza kuna kitu nataka nikwambie. Ushashuhudia muvi ngapi kali mwezi huu. Nataka nikuonyeshe moja ya stelingi anayeitwa Edward Charles Manyama.

Washiriki wa kwenye hiyo muvi ni Simba, Yanga, Azam na mitandao ya kijamii.

Stelingi kafanya yake, si unajua stelingi hauwawi! Kazi ipo. Usiku wa Jumamosi iliyopita stelingi Manyama ambaye ni mchezaji wa Ruvu Shooting aliwaendea hewani Simba. Akawaambia maneno matatu tu; “Yanga,Azam wananitaka.”

Mwanaspoti linajua kwamba beki huyo alifanya hivyo kwa vile Simba awali ilishazungumza naye na ikamwambia muda wowote wangemalizana.

Habari zisizo na shaka zinasema kwamba baada ya kuwaambia Simba hivyo, alienda mbali zaidi kuwahakikishia kwamba hajasaini na akawatumia hata nakala ya mkataba wake na Ruvu ambao unamalizika baada ya mechi ya mwisho ya ligi Julai 18 na kwamba wachangamke kumaliza dili hilo.

Habari hizo zinasema kwamba Simba walimtilia shaka kwamba baada ya kutoka Namungo alishasainishwa Azam akaambiwa akatulie Ruvu. Lakini inadaiwa kwamba Manyama aliwakatalia kabisa Simba na kuwaonyesha mkataba wake na Ruvu.

Advertisement

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema kwamba Manyama aliwapigia simu Jumatatu akiwa kwenye kambi ya Taifa Stars, akawaambia kwamba kuna mtu wa Yanga amekuja na yuko chumbani kwa mchezaji mmoja wa klabu hiyo aliyeko kambini hapo.

Habari zinasema kwamba baada ya kiongozi huyo wa Yanga kuona Manyama haendi akaenda kumgongea chumbani kwake mchezaji akatoka akamwambia “nakuja” ndipo akahama chumbani hapo ambapo alikuwa akilala na Idd Seleman ‘Nado’ wa Azam.

Mwanaspoti linajua kwamba Jumanne, kigogo mmoja wa Simba alimpigia Manyama na kwenda kumchukua mida ya saa 1 usiku baada ya kutoka kwenye mazoezi ya Stars.

Mchezaji huyo inadaiwa kwamba alikwenda kwa viongozi wa Stars waliokuwa kambini hapo na kuwaeleza juu ya ishu yake na Simba na akawaomba wampe dakika kadhaa akazungumze na Wekundu hao juu ya hatma yake na wakamruhusu.

Wawakilishi hao wa Simba walimbeba na gari aina ya Toyota Alphard kwa usiri mkubwa akaenda kwenye ofisi ya kigogo mmoja wa Simba iliyopo Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam umbali wa dakika 20 kutoka ilipo kambi ya Stars katikati ya Jiji.

Baada ya kufika eneo la tukio, Manyama akapewa mkataba wa Simba wenye karatasi zaidi ya 10 akazisoma kwa muda usiozidi dakika 15, akiwa amezungukwa na wazito kama watano wa Simba baadaye akasema sawa ndipo akasaini.

“Baada ya kusaini ndio likaanza zoezi la kupiga picha akiwa na jezi ya Simba, baada ya kumalizana akavaa jezi yake ya timu ya Taifa akarudishwa kambini.”

Mwanaspoti ambalo lilijiridhisha kwa kiwango cha juu kabisa, likarusha stori hiyo Jumatano wiki hii na hapo ndipo picha likaanza kwenye mitandao ya kijamiii na Azam wakaanza kutafutana. Ikaanza mijadala ya ndani ya kwenye klabu ya Azam kuhusiana na dili la Manyama, Alhamisi usiku wakaposti picha kwenye mitandao yao ya kijamii wakimuonyesha Manyama akiwa amevalia jezi Taifa Stars na kuandika; “Karibu Azam Fc.”

Taarifa ya Azam inasema kwamba Manyama amesaini miaka mitatu na Mwanaspoti pia linajua mchezaji huyo amesaini Simba miaka mitatu.

Kwenye akaunti zake binafsi za mitandao ya kijamii, Manyama hajaposti chochote kuhusiana na usajili wake Azam jambo ambalo limeibua mijadala midomoni mwa wadau huku wengine wakidai kwamba kuna namna.

Kanuni za usajili zinamruhusu mchezaji ambaye mkataba wake upo chini ya miezi sita kuzungumza na klabu mpya, lakini klabu yake inapaswa kupewa taarifa kabla ya hilo.

Hata hivyo, habari za chini chini zinasema juzi na jana vigogo wa Simba walikutana kujadili jambo hilo, hasa kutokana na uhusiano ulipo baina yao na Azam ili kuweka sawa jambo la Manyama.


WASIKIE WADAU

Godwin Aswile ‘Scania’ aliyetamba Tukuyu Stars, Simba, Yanga na Taifa Stars ni mhanga wa matukio hayo, kwani alijitolea mfano kilichomkuta msimu wa 1992/93 ambapo alieleza baada ya kucheza miaka sita Yanga na mkataba ulikuwa umemalizika aliwaaga viongozi kwa nia ya kutaka kuhamia Simba.

“Zamani mambo hayakuwa wazi, sikusaini Yanga, kwa vile walitaka niendelee kubaki, nami nilihitaji kucheza Simba, baada ya Simba kuonyesha mkataba na dole gumba nililoweka Yanga walikataa na kwamba wakapime Uingereza, hivyo na mwenzangu Thomas Kipese tukafungiwa kucheza mwaka mmoja Ligi Kuu,” alisema Aswile na kuongeza;

“Sheria zipo wazi, pia watafute mawakala ili kuepuka ushawishi na uongo wa viongozi ndipo wataweza kuwa salama.”

Naye beki wa zamani wa Simba, Frank Kasanga ‘Bwalya’ aliwapa tahadhari wachezaji; “Wachezaji wanatakiwa waangalie zaidi maisha kuliko tamaa zitakazoua ndoto zao, kama mchezaji ameamua kwenda kuichezea Yanga basi asaini Yanga, ama kaamua kusaini Simba basi asaini Simba tamaa ni mbaya na pia zinawaondoa kwenye heshima hata siku jambo hilo litakapoisha.”

Kocha wa zamani wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’ yeye alisema; “Mchezaji, soka ndio maisha yake yote yanategemea kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine, hivyo lazima atulize kichwa katika uamuzi waepuke tamaa, kwani inaweza kumharibia sifa na maisha yake yote ya baadaey. ”Beki huyo wa zamani wa Sigara, alisema msimu wa usajili wachezaji watafute sehemu watakayopata nafasi ya kucheza na maslahi pasi kukurupuka. “Wachezaji wengi wa Kitanzania wanaponzwa na kukosa elimu na washauri wazuri, inabidi waepuke vishawishi kwa kuangalia mbele zaidi nini wanakilenga,” alisema Cheche.

Julio naye alisema; “Mchezaji hawezi kusajiliwa timu mbili tofauti kama ilivyokuwa zamani na ikitokea hivyo, basi baina ya pande hizo tatu kuna mmoja atapata hasara au wawili kabisa.”

Advertisement