Prisons yaanza na Kalambo, Kisubi awaumiza vichwa

Muktasari:

  • Msimu uliopita Prisons ilimaliza nafasi ya saba kwa alama 42 na sasa wameanza kusuka upya kikosi ili kujiimarisha na msimu ujao.

Mbeya. Siku moja baada ya uongozi wa Tanzania Prisons kumtangaza Ally Mrisho kuwa Katibu Mkuu, kiongozi huyo ameanza kazi rasmi akimsainisha aliyekuwa Kipa wa Dodoma Jiji, Aaron Kalambo  huku akiahidi sura nyingine mpya kuanza kushushwa kikosini kuanzia  kesho Jumatatu.

Mrisho alitangazwa jana Jumamosi akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Ajabu Kifukwe ambaye amepangiwa majukumu mengine, akitokea timu ya Magereza inayoshiriki ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam alipokuwa akihudumu kama Katibu Mkuu.

Akizungumza na Mwanaspoti leo asubuhi Julai 25, Mrisho amethibitisha kumnasa Kalambo kwa mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa baada ya kumalizana na Kipa huyo ambaye aliwahi kukipiga kwa Maafande hao huko nyuma, sura nyingine mpya zitaanza kuonekana kuanzia kesho Jumatatu baada ya kikao cha viongozi na benchi la ufundi.

"Tumeanza na Kalambo ambaye ni kama karudi nyumbani, lakini hatuishii hapo kwani kuanzia kesho Jumatatu tutajurishana nani anaingia au kutoka baada ya kikao cha viongozi na benchi la ufundi" amesema Mrisho.

Katibu huyo pia amesisitiza kuwa licha ya Kipa wao, Jeremiah Kisubi kumaliza mkataba huku kukiwa na tetesi za kusajiliwa na moja ya klabu kubwa hapa nchini, lakini bado wanamuona kama mali yao hadi sasa na huenda akaongezewa muda kubaki kikosini.

"Bado yupo kwenye rada zetu Kisubi, tusubiri muda utaamua..kujua wangapi tutasajili au kuacha itajulikana kesho lazima tutatoa taarifa mapema ili kila mmoja awe na uhakika" amesema Katibu huyo.