Profesa Mkenda aahidi jezi, mipira kwa timu 59 Rombo
Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu nchini Tanzania,Profesa Adolf Mkenda akimpa mpira Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Rombo ,John Kanyau kabla ya uzinduzi wa Bonanza la mpira"mbunge cup" haujaanza.picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda ameahidi kutoa jezi pamoja na mipira kila mwaka timu 59 za mpita wa miguu zitakavyofanya vizuri wilayani humo ili kuendeleza mchezo wa soka vijana.
Rombo. Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda ameahidi kutoa jezi pamoja na mipira kila mwaka kwa vilabu 59 vya michezo vitakavyofanya vizuri wilayani humo ili kuendeleza mchezo wa soka vijana.
Profesa MKenda ameyasema hayo leo Januari 24, 2022 wakati wa uzinduzi wa mashindano ya "Mbunge Cup" yaliyokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyoadhimishwa na Umoja wa vijana wa UVCCM wilayani humo.
Aidha amewataka wadau wa maendeleo wilayani humo kujitokeza na kuunga mkono jitihada za kuendeleza michezo wilayani humo ili kuhakikisha mabingwa wa ligi kuu wanapatikana katika wilaya hiyo.
"Ndugu zangu michezo ni ajira, tukiendeleza tasnia ya michezo katika wilaya hii vijana mtapata ajira na ndio maana leo hii tunaona ndugu zetu wa UVCCM wameamua kuadhimisha miaka 45 ya CCM kwa michezo," amesema Profesa Mkenda.
Ameongeza; "Timu itakayofanya vizuri hapa Rombo na mimi kama Mbunge wa Rombo naahidi kila mwaka tutaunga mkono jitihada hizi, tutaleta jezi, mipira, makombe na tutapigania maeneo mengi zaidi ya kufanya mazoezi kwa vijana wetu," amesema Profesa Mkenda.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM wilaya hiyo, John Kanyau amesema baada ya uzinduzi wa bonanza hilo la michezo wilayani humo wataanza kucheza kwa ngazi za kata na mashina ili kumpata bingwa wa Wilaya.
"Leo tumeadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi (CCM), baada ya uzinduzi huu timu zitaanza kucheza kwa ngazi za mashina, kata na hatimaye tutapata bingwa wa wilaya ya Rombo," amesema.
Ameongeza; "Bingwa wa Wilaya zawadi yake itakuwa Sh2milioni pamoja na kombe, mshidi wa pili Sh1milioni, watatu Sh500,000 na mshindi wa nne Sh250,000 na timu zote zitakazoshiriki zitapewa jezi moja moja pamoja na mipira," amesema Kanyau.