Tahadhari ya Polisi kwa Yanga, Azam kesho
Kamanda wa Jeshi la Polisi, Wilbrod Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza. Picha na Polisi
Muktasari:
- Kwa wapenzi wa michezo wajiepushe na vitendo vya fujo na uvunjifu wa amani kabla, wakati na baada ya mchezo huo, na yeyote atakayebainika kuanzisha vurugu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema limeimarisha usalama kuelekea mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kati ya Yanga na Azam FC.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho Juni 21, 2026, saa 9:30 alasiri katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Jana Ijumaa 19, 2026, Kamanda wa Jeshi la Polisi, Wilbrod Mutafungwa amesema Ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unakuwepo wakati wote, jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kwa kuimarisha mifumo ya kiusalama maeneo yote ya ndani na nje ya uwanja.
“Katika kufanikisha azma hiyo, Jeshi la Polisi linatoa tahadhari kuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kuingia au kusogea karibu na uwanja huo akiwa na silaha ya aina yoyote, ikiwemo silaha za moto, silaha za jadi, au kifaa chochote chenye ncha kali kinachoweza kutumika kuumiza watu. Isipokuwa kwa baadhi ya askari watakaokuwa na jukumu la kulinda usalama eneo hilo,” amesema Mutafungwa
Amesema kwa wapenzi wa michezo wajiepushe na vitendo vya fujo na uvunjifu wa amani kabla, wakati na baada ya mchezo huo, na yeyote atakayebainika kuanzisha vurugu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Jeshi la Polisi linazitakia kila la heri timu zote mbili na kuwataka mashabiki kukubali matokeo yoyote yatakayotokea uwanjani kwa mujibu wa sheria za soka, kwani soka ni burudani, urafiki, na undugu.
Mashabiki wamesema kwenye mchezo huo watashabikia kwa amani na kufurahia burudani itakayotolewa bila kuleta vurugu.
Samweli Mkuya shabiki anasema, “mchezo wa mpira una matokeo matatu kwa hiyo tuko tayari kuyapokea lakini ushindi tunategemea zaidi alama tatu lazima.”
Joseph Msukuma anasema, “vurugu ambazo huwa zinatokea hazifurahishi. Zinapoteza kwanza ladha ya burudani uwanjani. Nashauri tu mashabiki wenzangu tuwe waungwana ili turudi salama majumbani kwetu.”