Dakika mbili za maajabu Yanga ikirejea kileleni
Muktasari:
- Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 66 na kuendelea kujikita kileleni, baada ya kushinda mechi 20, sare sita na kupoteza moja, huku kwa upande wa Fountain ikiwa nafasi ya 10 na pointi 29, ikishinda nane, sare tano na kupoteza 14.
Dar es Salaam. Dakika mbili za maajabu zimetosha kuirudisha tena Yanga kileleni kibabe baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Fountain Gate, katika mechi kali ya kuvutia ya Ligi Kuu, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha.
Mabao mawili ya dakika mbili kutoka kwa kiungo, Pacome Zouzoua dakika ya 52 na mshambuliaji, Laurindo Dilson Maria 'Depu' dakika ya 54 yalitosha kuirejesha Yanga kileleni na kuishusha tena Simba iliyodumu kwa sasa 24 tu.
Kabla mechi hiyo Simba ilikuwa kileleni baada ya kuifunga Mbeya City bao 1-0, kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini, Mbeya na kufikisha pointi 64, japo ushindi wa Yanga umeirejesha kileleni kwa tofauti ya pointi mbili kufuatia kuwa na pointi 66.
Bao hilo la Pacome ni la nane katika Ligi Kuu kwa nyota huyo baada ya kukaa kwa muda mrefu bila ya kufunga tangu mara ya mwisho alipokifungia kikosi hicho mabao yake mawili katika ushindi mnono wa 6-0, dhidi ya Mbeya City, Aprili 16, 2026.
Kwa upande wa Depu amefikisha mabao saba ya Ligi Kuu Bara tangu ajiunge na kikosi hicho dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Radomiak Radom FC ya Poland, baada ya ukame wa muda mrefu tangu mara ya mwisho kwake alipofunga Machi 12, 2026.
Kabla ya bao hilo, mara ya mwisho kwa nyota huyo raia wa Angola kufunga ilikuwa ni ushindi wa timu hiyo wa 1-0, dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma Machi 12, 2026.
Yanga inayopambana kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara iliochukua kwa misimu minne mfululizo, iliingia katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu nzuri baada ya raundi ya kwanza kuifunga pia Fountain Gate mabao 2-0, Desemba 4, 2025.
Kwa upande wa Fountain Gate iliingia katika mechi hiyo ikihitaji kulipa kisasi cha kufungwa na Yanga lakini pia mara ya mwisho kwenye Uwanja wa Sheikh Amri, Abeid Arusha ilishindwa kutamba baada ya kuchapwa na Azam mabao 2-0, Juni 12, 2026.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 66 na kuendelea kujikita kileleni, baada ya kushinda mechi 20, sare sita na kupoteza moja, huku kwa upande wa Fountain ikiwa nafasi ya 10 na pointi 29, ikishinda nane, sare tano na kupoteza 14.
MATOKEO MENGINE
Mechi nyingine iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, JKT Tanzania ilishindwa kutamba mbele ya maafande wenzao wa Tanzania Prisons, baada ya kuchapwa bao 1-0, lililofungwa na nyota, George Mpole kwa mkwaju wa penalti ya dakika ya 45.
Ushindi huo ni wa tatu mfululizo kwa Prisons baada ya kuifunga Pamba Jiji mabao 3-2, kisha kuichapa pia Dodoma Jiji 3-1 na kusogea kutoka nafasi ya 15 hadi ya 14 na pointi 26 ambazo zinaiweka nafasi nzuri ya kuepuka janga la kushuka daraja.
Nafasi hiyo ya 14 kwa Prisons inaweka katika nafasi ya kucheza Play-Off huku ikiiachia Mbeya City msala kwa kushuka hadi nafasi ya 15 na pointi 25, huku kwa upande wa JKT Tanzania ikiendelea kusalia nafasi yake ya sita na pointi zake 38.
Katika mechi nyingine iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ilishuhudiwa Pamba Jiji ikishinda mabao 4-0, dhidi ya Mtibwa Sugar huku nyota wa kikosi hicho, Mkenya Mathew Momanyi akifunga Hat-Trick ya pili ya Ligi Kuu kwa msimu huu.
Hat Trick hiyo ya Momanyi inakuwa ya pili msimu huu katika Ligi Kuu, baada ya nyota Singida Black Stars, Mrundi Mossi Nduwumwe kutangulia kufunga ya kwanza katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 5-0, dhidi ya Dodoma Jiji, Juni 17, 2026.