PSG yaifuata Arsenal fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya
Mshambuliaji wa PSG, Ousmane Dembele akishangilia baada ya kufunga moja ya bao katika sare ya 1-1 kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, Mei 6, 2026. Picha na Mtandao
Muktasari:
- PSG imeingia katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya tatu huku ikifanya hivyo mara mbili mfululizo baada ya kutwaa taji hilo msimu uliopita.
Munich, Ujerumani. Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, PSG, wametinga tena fainali ya michuano hiyo ambapo watakutana na Arsenal, baada ya kuiondoa Bayern Munich kwa jumla ya mabao 6-5 katika dakika 180 za nusu fainali.
Ousmane Dembele alifunga bao lililogeuka kuwa la ushindi katika dakika ya 3, mechi iliyochezwa jijini Munich nchini Ujerumani, Jumatano Mei 6, 2026, akiipa PSG uongozi wa mabao mawili kwa jumla, kufuatia ushindi wa 5-4 walioupata katika mchezo wa kwanza wiki iliyopita.
Hatimaye Harry Kane aliifungia Bayern Munich, kama ilivyo kawaida yake (akiwa na mabao 14 katika mechi 13 ya Ligi ya Mabingwa msimu huu), lakini bao hilo lilikuja kuchelewa mno katika dakika ya 94.
Bao la PSG lilipatikana baada ya Khvicha Kvaratskhelia kutoa pasi ya chini ndani ya eneo la hatari, iliyomkuta Ousmane Dembele aliyepiga shuti kali na kufunga.
Bayern walijibu kwa kasi na walikaribia kusawazisha katika dakika ya 27, pale Harry Kane alipompa pasi Michael Olise, ambaye alipiga shuti lililopita kidogo juu ya lango.
Unaweza kusema Bayern walinyimwa penalti dakika ya 30, kufuatia mpira wa Vitinha kugonga mkono wa Joao Neves, ambao ulionekana kuwa katika nafasi ya kawaida.
Baadaye, Neves alimlazimisha kipa Manuel Neuer kufanya kazi ya ziada, akidaka kwa ustadi kichwa chake na kuokoa hatari.
Bayern walimaliza kipindi cha kwanza kwa nguvu, huku Jamal Musiala akimlazimisha kipa Matvey Safonov kufanya sevu mbili mfululizo, kabla ya Jonathan Tah kukosa nafasi nzuri ya kufunga kwa kichwa.
Kipindi cha pili kilianza kwa Neuer kuokoa shuti la Desire Doue karibu na goli, kabla ya kuzuia kwa mguu shuti lingine la Kvaratskhelia muda mfupi baadaye.
Neuer aliendelea kung’ara dakika ya 63 kwa kuokoa kwa kujirusha shuti la Doue lililokuwa liwe bao la pili.
Upande wa Bayern, Luis Diaz na Olise waliendelea kushambulia na kumlazimisha Safonov kufanya save kadhaa walipokuwa wakisaka bao la kusawazisha.
Kvaratskhelia alikaribia kumaliza kabisa matumaini ya Bayern baada ya kupenya peke yake, lakini alishindwa kuumudu mpira vizuri na kuruhusu Min-Jae Kim kuondoa hatari.
Hatimaye Kane alisawazisha katika dakika za nyongeza, lakini ilikuwa ni kuchelewa mno kwa Bayern kukamilisha kurejea kwao.
Ushindi huo wa PSG unaifanya kwenda kupambana na Arsenal katika fainali ya michuano hiyo iliyopangwa kuchezwa Mei 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Puskas uliopo Budapest nchini Hungary.