Ratiba EPL yaanikwa, Arsenal kufungua dimba
Muktasari:
- Msimu wa Ligi Kuu England utaanza rasmi Ijumaa, Agosti 21, 2026 na utafikia tamati Jumapili, Mei 30, 2027.
Ratiba ya Ligi Kuu England 2026/2027 imetolewa rasmi leo Ijumaa, Juni 19, 2026 ikitarajiwa kuanza Agosti 21, 2026 na kumalizika Mei 30 mwakani.
Pazia la ligi hiyo litafunguliwa kwa mchezo baina ya bingwa mtetezi Arsenal dhidi ya Coventry City utakaochezwa Ijumaa, Agosti 21, 2026 katika Uwanja wa Emirates ambapo Arsenal atakuwa mwenyeji.
Washindi wa pili wa msimu uliomalizika, Man City wataanzia nyumbani dhidi ya Bournemouth, Agosti 23 na washindi wa tatu wa msimu ulioisha, Man United watakuwa ugenini kucheza na Hull City, Agosti 22.
Liverpool itaanzia ugenini dhidi ya Newcastle United, Chelsea nayo itaanzia ugenini dhidi ya Fulham kama ilivyo kwa Totteham Hotspur ambayo itakuwa katika uwanja wa ugenini kukabiliana na Brentford.
Mashabiki wa ligi hiyo watapata uhondo wa mechi kubwa katika raundi ya tatu tu ya msimu ujao, ambapo Arsenal itakabiliana na Chelsea.
Mechi hiyo itachezwa Jumamosi, Septemba 5, 2026 ambapo Arsenal itakuwa mwenyeji.
Kabla hawajapoa, mashabiki hao katika raundi inayofuata watashuhudia mtanange wa watani wa jadi wa jiji la Manchester, baina ya Man United na Man City.
Mechi hiyo baina ya Manchester United na Manchester City itachezwa Jumamosi, Septemba 12, 2026 katika Uwanja wa Old Trafford.
Raundi ya sita itakuwa na mechi nyingine kubwa ambayo ni baina ya Liverpool na Manchester City itakayochezwa, Jumamosi, Oktoba 10, 2026.
Liverpool itakuwa ni mwenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa, katika Uwanja wa Anfield.