Robertinho afichua siri za Baleke
Muktasari:
- Kocha Robert Oliviera ‘Robertinho’ amewasisitiza mabosi wa klabu hiyo kama kuna vita wanatakiwa kupigana nyakati hizi ni kumbakisha Baleke Simba baada ya moto wake wa kupiga mabao.
KAMA kuna jina likitajwa linawashtua mashabiki wa Yanga basi ni mshambuliaji Jean Baleke ambaye ameuwasha moto mkali wa kupiga mabao na sasa kocha wake amewapa mabosi wa klabu hiyo ramani ya kutaka kumwona zaidi ndani ya timu hiyo.
Kocha Robert Oliviera ‘Robertinho’ amewasisitiza mabosi wa klabu hiyo kama kuna vita wanatakiwa kupigana nyakati hizi ni kumbakisha Baleke Simba baada ya moto wake wa kupiga mabao.
Robertinho alisema Baleke ambaye anaitumikia Simba kwa mkopo wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwaka mwingine amezungumza naye na kwa sasa hataki kurudi tena kirahisi klabu yake TP Mazembe akitaka kuendelea kuvaa jezi za Wekundu hao kutokana na mzuka mkubwa alioanza nao.
Mpaka sasa Baleke ameifungia Simba jumla ya mabao 14 kwenye mashindano yote yakiwemo saba ya Ligi Kuu Bara, matatu akifunga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku manne akifunga Kombe la Azam Shirikisho.
“Huyu ni mfungaji wetu bora mpaka sasa lakini kitu bora zaidi amekuwa na furaha na bahati akiwa na Simba, nimeongea naye anataka sana kubaki hao kwa kuwa ameanza vizuri nafikiri itakuwa hatua nzuri kwa uongozi kupambana kumbakisha hapo kwa muda zaidi,” alisema Robertinho.
“Wakati anafika nilimwambia ni uamuzi kwake kama anataka mafanikio na hii sio tu kwa Baleke hata Phiri (Moses), Habib (Kyombo), Bocco (John) na wengine, kitu muhimu ni kujituma kuanzia mazoezi na kwenye mechi.
Aidha Robertinho alisema silaha kubwa ya Baleke ni utulivu wake anapokuwa ndani ya eneo la hatari na amemwambia akiendelea kutulia zaidi ataishangaza Tanzania kwa kufunga zaidi.
Alisema ushindi wao dhidi ya Ihefu ugenini uliotokana na mabao ya Mkongomani huyo yatakuwa morali kubwa kwa timu yake na mashabiki kuelekea mchezo dhidi ya Yanga, Jumapili Aprili 16.
“Mabadiliko tuliyoyafanya kwenye mchezo wa jana (juzi) na tukashinda hii ni uthibitisho mkubwa wachezaji wanaendelea kubadilika kwa haraka, mimi napenda namna hii kwani itaongeza ushindani zaidi.
“Huu ni ushindi muhimu unapoelekea mchezo mkubwa, tutaingia kwenye maandalizi dhidi ya Yanga tukiwa na morali kubwa, pia hata mashabiki wetu watakuja kuipa nguvu timu yao wakiwa na furaha na nguvu kubwa.
Simba imerejea jana usiku jijini Dar es Salaam ikitokea Mbeya iliposhinda kwa mabao 2-0 na kuendelea kuwafukuza watani wao Yanga ambao wako juu ya msimamo wa ligi.