Ronaldo asalia Saudi Arabia, Al-Nassr yatoa ufafanuzi
Muktasari:
- klabu hiyo imetangaza kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 41 anasumbuliwa na majeraha ya msuli wa paja aliyoyapata Jumamosi katika mechi dhidi ya Al-Fayha.
Riyadh, Saudi Arabia. Klabu ya Al-Nassr imethibitisha kuwa nahodha wake, Cristiano Ronaldo, bado yupo Saudi Arabia, ikikanusha tetesi zilizoenea kuwa ameondoka Mashariki ya Kati kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi katika ukanda huo.
Tetesi hizo zilianza baada ya ndege yake binafsi yenye thamani ya pauni 61 milioni (Sh180 bilioni) kuonekana ikiondoka Saudi Arabia usiku wa manane kuelekea jijini Madrid, Hispania.
Hata hivyo, Al-Nassr ilichapisha picha mtandaoni zikimuonesha Ronaldo akiwa katika viwanja vya mazoezi vya klabu hiyo pamoja na wachezaji wenzake, kuthibitisha kuwa bado yupo nchini humo.
Wakati huo huo, klabu hiyo imetangaza kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 41 anasumbuliwa na majeraha ya msuli wa paja aliyoyapata Jumamosi katika mechi dhidi ya Al-Fayha.
Nyota wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo, anaripotiwa kuwa bado yupo Saudi Arabia akiendelea na mazoezi kwenye Klabu yake. Picha na Mtandao
Katika taarifa fupi, Al-Nassr imesema:
“Cristiano Ronaldo amegundulika kuwa na majeraha ya msuli wa paja baada ya mchezo uliopita dhidi ya Al-Fayha. Ameanza programu ya matibabu na atafuatiliwa siku hadi siku.”
Ronaldo anayelipwa kiasi cha Sh1.7 bilioni kwa siku katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia, alitolewa nje katika ushindi wa mabao 3-1, na sasa kuna hofu juu ya ukali wa jeraha hilo hasa ikizingatiwa kuwa Kombe la Dunia linakaribia.
Mshambuliaji wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo, wakati akipiga mkwaju wa penalti ambao ulipita nje ya lango katika mechi ya Ligi Kuu Saudi Arabia dhidi ya Al-Fayha. Picha na Mtandao
Mechi za Asia zaahirishwa
Kutokana na hali ya usalama, mchezo wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Asia kati ya Al-Nassr na Al-Wasl umeahirishwa. Shirikisho la Soka la Asia (AFC) limetangaza kuahirisha mechi kadhaa za kanda ya Magharibi hadi hapo hali itakapokaa sawa.
Riyadh, ambako Ronaldo anaishi pamoja na mwenzi wake Georgina Rodriguez na watoto wao watano, imeripotiwa kulengwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Ndege binafsi ya mshambuliaji wa Ureno na Al-Nassr, Cristiano Roanldo ambaye bado hajajulikana kama ameondoka Saudi Arabia baada ya kuibuka kwa machafuko huko Mashariki ya kati. Picha na Mtandao
Taharuki ya usafiri
Kwa mujibu wa taarifa za ufuatiliaji wa safari za ndege, ndege binafsi ya Ronaldo aina ya Bombardier Global Express 6500, imesafiri takribani saa saba hadi Madrid.
Ndege hiyo ya kifahari ina uwezo wa kubeba abiria 15 na ina vyumba vya kifahari, ikiwamo sehemu ya mapumziko, kitanda cha watu wawili na bafu maalumu.
Pia imepambwa kwa nembo yake binafsi na picha ya umbo lake akishangilia bao.
Mashambulizi ya pamoja ya Israel na Marekani dhidi ya Iran yameripotiwa kusababisha vifo vya viongozi wa ngazi za juu. Picha na Mtandao
Wakati huo huo, Marekani chini ya Rais Donald Trump, imetoa tahadhari kwa raia wake kuondoka katika baadhi ya mataifa ya Mashariki ya Kati kutokana na hatari za kiusalama. Milipuko mikubwa imeripotiwa kusikika katika miji ya Ghuba huku hali ya taharuki ikiongezeka.
Kuongezeka kwa mapigano kumesababisha usumbufu mkubwa wa safari za anga na shughuli za kijamii katika ukanda huo, huku mashabiki na wachezaji wakisubiri maamuzi zaidi kuhusu usalama wao.