Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu Guardiola kuiongoza Man City fainali ya Carabao na kifungo

Muktasari:

  • Guardiola ataendelea kuwa benchi katika fainali ya Kombe la Carabao itakayopigwa Machi 22 dhidi ya Arsenal.

Manchester, England. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, atakuwa sehemu ya benchi la ufundi kuiongoza timu yake katika fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Arsenal licha ya kukabiliwa na adhabu ya kufungiwa mechi mbili.

Guardiola alipata kadi yake ya sita ya njano msimu huu wakati City walipoifunga Newcastle United mabao 3-1 katika raundi ya tano ya Kombe la FA mwishoni mwa wiki.

Kocha huyo Mhispania alipoteza utulivu baada ya kumlalamikia mwamuzi kufuatia tukio ambalo beki wa Newcastle, Kieran Trippier, alionekana kumvuta mshambuliaji wa City, Jeremy Doku.

Katika tukio hilo, Guardiola alionekana kumkabili mwamuzi wa nne Lewis Smith kwa hasira huku akivua koti lake kwa ghadhabu, na hata baada ya mechi alilazimika kuzuiliwa alipokuwa akijaribu kwenda kuzungumza na maafisa wa mchezo.

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, wakati alipokuwa akilalamika dhidi ya maamuzi ya Refa. Picha na Mtandao


Adhabu haitahusu fainali

Kwa mujibu wa kanuni za msimu huu, kadi ya sita ya njano inamaanisha kocha huyo atafungiwa kusimama benchi katika mechi mbili.

Hata hivyo, adhabu hiyo inahusu mechi za Ligi Kuu England na Kombe la FA pekee, na haihusishi fainali za vikombe vya ndani au mashindano ya Ulaya.

Hivyo, Guardiola ataendelea kuwa benchi katika fainali ya Kombe la Carabao itakayopigwa Machi 22 dhidi ya Arsenal.

Badala yake, atalazimika kutazama kutoka jukwaani katika mchezo wa ligi dhidi ya West Ham United, pamoja na mechi ya robo fainali ya Kombe la FA inayotarajiwa kupigwa mwanzoni mwa Aprili.

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, wakati alipokuwa akilalamika dhidi ya maamuzi ya Refa. Picha na Mtandao


Guardiola ajitetea

Akizungumzia tukio hilo, Guardiola amesema alikuwa anamtetea mchezaji wake.

“Jeremy Doku alipompita Trippier na kuelekea langoni, alivutwa kutoka nyuma. Sikuwa naomba kadi ya njano, lakini ilikuwa faulo. Nitaitetea timu yangu,” amesema.

Kwa utani, Guardiola pia amesema adhabu hiyo inaweza kumpa nafasi ya kwenda likizo kwa muda mfupi.

“Nimefungiwa mechi mbili sasa, nitaenda likizo katika mechi hizo mbili,” amesema kwa kejeli.

Iwapo Guardiola atapata kadi tisa za njano msimu huu, atafungiwa mechi tatu, huku kadi 12 zikimuweka hatarini kushtakiwa kwa utovu wa nidhamu.