Sababu kocha Azam kukosa tuzo yatajwa

Muktasari:

  • BODI ya Ligi (TPBL) leo Desemba 8 imetangaza washindi wa tuzo za mwezi Novemba na maswali yakiibuka baada ya kutoonekana kwa jina la Kocha wa Azam FC, Kally Ongala licha ya kuwa na rekodi nzuri ndani ya kikosi hicho.

BODI ya Ligi (TPBL) leo Desemba 8 imetangaza washindi wa tuzo za mwezi Novemba na maswali yakiibuka baada ya kutoonekana kwa jina la Kocha wa Azam FC, Kally Ongala licha ya kuwa na rekodi nzuri ndani ya kikosi hicho.

Tuzo hizo ambazo zinatolewa na Bodi ya Ligi, zinatolewa kila mwezi kwa wachezaji, makocha na mameneja wa uwanja kutokana na rekodi zao kwa mwezi husika.

Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amechaguliwa kocha Bora wa mwezi Novemba 2022 katika Ligi Kuu ya NBC akiwashinda Hans Pluijm (Singida Big Stars) na Mecky Maxime (Kagera Sugar).

Naye mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba 2022, akiwapiku Moses Phiri (Simba) na Saido Ntibanzokinza (Geita Gold).

Taarifa ya bodi imejibu maswali ya kwanini Kocha Ongala hakutajwa kwenye tuzo hizo ikisema,"Kamati ya tuzo ya TFF katika kikao chake upande wa mchakato wa kocha bora wa mwezi, haikuhusisha timu ya Azam FC kutokana na kutokuwa na kocha mkuu kwa mwezi Novemba."

Aidha Mwanaspoti limemtafuta Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda amesema sababu ya kocha wa Azam kutohusishwa kwenye tuzo hizo ni kwasababu timu hiyo ilikuwa haina kocha mkuu na kocha aliyekuwepo hana vigezo.

"Taarifa ya Azam kutohushwa kwenye tuzo za mwezi ni kwasababu timu hiyo ilikuwa haina kocha mkuu na kocha aliyekuwepo hana vigezo vya kuwa kocha mkuu wala kocha msaidizi na hatujakosea kwenye kufanya maamuzi katika hilo," alisema Boimanda.

Ongala alikabidhiwa mikoba ya kukinoa kikosi hicho mwezi Oktoba baada ya kumtimua Dennis Lavagne na kukiongoza katika mechi nane za ligi bila kupoteza.

Azam chini ya Ongala imepata ushindi dhid ya Simba, Ihefu, Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting, Namungo,  Coastal Union na Polisi  Tanzania.

Pia kamati ya tuzo ilimchagua Hassani Simba kuwa meneja bora wa Uwanja wa Liti uliopo mkoani Singida.