Sababu tatu zilizoondoa vigogo Simba

Dar es Salaam. Usajili usio wa kuridhisha wa wachezaji na makocha, kufanya vibaya kwa misimu mitatu mfululizo pamoja na ucheleweshaji wa klabu kuingia kwa asilimia mia kwenye mfumo wa uwekezaji ni sababu tatu zilizomfanya Mwekezaji wa Simba Mohamed Dewji Mo kuwataka wajumbe wa bodi upande wake kujiuzulu kwa mpigo.

Wajumbe watano tayari wameshaachia ngazi, huku mmoja akiwa bado, lakini ikielezwa kuwa mustakabali wake utajulikana siku chache zijazo.

Watano hao ni kati ya sita ambao waliteuliwa na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji na aliyebakia ni mmoja tu ambaye ni Salim Abdallah 'Try Again' ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo.

Watano hao ambao wameamua kujiweka pembeni ni Raphael Chegeni, Hamza Johari, Zulfikar Chandoo, Rashid Shangazi na Hussein Kita.

Inaripotiwa kuwa vigogo hao wameamua kujiwajibisha kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika miaka ya hivi karibuni ambapo kwa kipindi cha misimu mitatu mfululizo, imeshindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na ule wa Kombe la Shirikisho la Azam huku mara kadhaa ikiishia hatua ya robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika.

Lakini pia mwekezaji wa timu hiyo, Mohammed Dewji inaripotiwa hajafurahishwa na usajili wa wachezaji mbalimbali uliofanywa na timu hiyo katika kipindi hicho sambamba na kuchelewa kukamilisha mchakato wa mabadiliko, jambo analoamini limechangiwa na kutokuwepo na usimamizi mzuri kutoka kwa bodi ya wakurugenzi.

 Wakati ikielezwa kuwa kila mmoja alipigiwa Simba na Mo na kutakiwa kujiuzulu, Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi ambaye ni mmoja wa wajumbe wa upande wa mwekezaji huyo waliojiuzulu, alisema jana kuwa wameamua kufanya hivyo ili kumpa nafasi Dewji kuingiza sura mpya.

"Nimefanya hivyo kama sehemu ya uwajibikaji kwa namna ambavyo hatukuwa na matokeo mazuri katika takribani misimu hii miwili. Mimi kama kiongozi nimejitathmini nimeona kwamba inawezeka kuna mahali hatukufanya vizuri sana basi uungwana ni kupisha ili mwenyekiti na mwekezaji wetu aweze kutengeneza safu upya ya bodi ambayo itakwenda kuisimamia Simba SC iweze kuwa klabu irudishe utimamu wake katika kuchukua vikombe.

"Neno moja kwa wanachama, Uongozi ni kupokezana na uongozi unahitaji mshikamano na nguvu ya pamoja. Wasiiache timu na waendelee kuisapoti wakati wote. Haswa kipindi hiki ambacho tupo katika mapitio. Sisi tumewajibika ili tuweze kujipanga upya lakini tutakuwa na mchango ambao tutaendelea kuutoa kwenye timu kwa kadri inavyohitajika," alisema Shangazi.

Pamoja na kwamba Dewji aliwateua mwenyewe wajumbe hao, uamuzi wa kuwaomba wajiuzulu ameuchukua ili kutokiuka katiba ya klabu hiyo ambayo inafafanua kuwa mjumbe wa bodi atakoma kutumikia nafasi yake ikiwa mambo manne yatatokea.

"Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi aliyechaguliwa na kuteuliwa kwa mujibu wa ibara ya 27 ya katiba hii atakoma kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi iwapo atatenda au kufanya mojawapo ya mambo yafuatayo. (a) Kujiuzulu kwa maandishi na kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa bodi ya wakurugenzi. (b) Kutohudhuria mikutano minne mfululizo ya kawaida ya bodi ya wakurugenzi. (c) Anashindwa kutekeleza majukumu ya mjumbe kutokana na kuumwa au sababu nyingine yoyote kwa kipindi cha miezi 12 mfululizo," inafafanua ibara ya 29 ya katiba hiyo.

Katika kuhakikisha Simba inakuwa imara msimu ujao, Dewji anatajwa kufanya maamuzi kadhaa ambayo anaamini yanaweza kuirudisha makali yake na kuepuka kile kilichotokea hapo nyuma.

Miongoni mwa hayo ni kuwa mstari wa mbele ni kushiriki kwa ukaribu mchakato wa usajili wa nyota wapya ambao wataitumikia klabu hiyo ikiripotiwa kwamba hakuridhishwa na namna timu hiyo ilivyokuwa ikiendesha zoezi hilo kwa miaka ya hivi karibuni.

Na katika kuhakikisha hilo linafanyika kwa umakini na ubora wa hali ya juu, Dewji ameamua kuwaongeza watu wanne wazoefu wa masuala ya usajili kusimamia zoezi hilo ambao ni Simba imeshawarudisha Crecensius Magori, Mulamu Nghambi, Kassim Dewji na Sued Mkwabi.

Ikumbukwe wakati Magori akiwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo ndio aliifanya iwe na kikosi tishio akisajili nyota kama Clatous Chama, Luis Miquissone, Meddie Kagere na Pascal Wawa.

Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally aliwahi kunukuliwa akithibitisha kuwa mchakato wa usajili ni zoezi litakalosimamiwa na Dewji mwenyewe.

"Fedha yote ya usajili ya msimu ujao atatoa Dewji, na mzigo ambao umetengwa kwa ajili ya usajili ni mkubwa. Niwaambie, Mo tunaye sana na tunatamba naye, usajili huu unaokuja utausimamia mwenyewe kwa asilimia mia moja.

"Kwa hiyo wanachama na mashabiki msiwe na wasiwasi, atasimama mwenyewe kwa miguu miwili kuhakikisha wachezaji bora na wa gharama wanatua kwenye klabu hii, mateso, manung'uniko, masononeko sasa basi," alisema Ally.

Dewji pia anasimamia mwenyewe mchakato wa kocha mpya, ambapo inaelezwa kuwa ameshakutana na mmoja nchini Dubai alipo kwa sasa akitaka timu hiyo iende kwenye maandalizi ya msimu katikati ya mwezi ujao.