Try Again ajiuzulu Simba, Barbara ndani

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salum Abdallah 'Try Again' anayedaiwa kujiuzulu.

Muktasari:

  • Baada ya kuwa na msimu mbaya, klabu ya Simba imeanza kufanya mabadiliko ya uongozi ambapo inadaiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salum Abdallah Muhene 'Try Again' pamoja na safu yake wamejiuzulu.

Dar es Salaam. Inadaiwa kuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi upande wa Mwekezaji Mohamed Dewji wameachia ngazi.

Taarifa zinasema kuwa MO amewapigia wajumbe wake wote akiwataka waandike barua za kujiuzulu kwa lengo la kuunda safu mpya ya uongozi kabla ya kuanza mchakato wa usajili mpya.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwananchi kuwa ni viongozi wote wa bodi ya Simba wametii wito wa kiongozi wao ambaye ndiye aliyewateua kwenye bodi hiyo.

“Hadi sasa ni wajumbe wote tayari wamejiuzulu kama mambo yataenda sawa kesho au keshokutwa Barbara Gonzalez atatangazwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi wa muda wa timu hiyo ili mambo yaende.

“Simu hizo amepiga kwa wajumbe wa upande wake pekee kwani ndio ambao anauwezo wa kufanya uamuzi huku kwa upande wa klabu viongozi waliopitishwa na wanachama kwenye mkutano mkuu wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.” kimesema chanzo hicho.

Wajumbe hao wa Bodi waliokuwa chini ya Mwenyekiti, Salum Abdallah Muhene 'Try Again'

ni Dk Raphael Chageni, Hamza Johari, Zulfikar Chandoo na Rashid Shangazi.

Hata hivyo, chanzo hicho kinasema baada ya kuingia mwenyekiti mpya timu hiyo itaanza harakati za usajili na kutafuta kocha mpya wa timu hiyo.

Mabadiliko hayo yanatokana na timu hiyo kuwa na msimu mbaya baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye ligi kitu ambacho hakijazoelekezaka kwa miaka zaidi ya 20.

Simba msimu ujao itashiriki kombe la Shirikisho pamoja na Coastal Union huku Yanga na Azam wakicheza Ligi ya Mabingwa.