Sakata la kuondolewa madarakani uongozi Yanga liko hivi

Mkurugenzi wa Sheria wa Klabu ya Yanga, Simon Patrick wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam. Picha na Yanga
Muktasari:
- Wakili wa Yanga, Simon Patrick amesema kufuatia hukumu iliyotolewa, uongozi wa timu hiyo umejipanga kufanya mambo matano sakata la akina Magoma.
Dar es Salaam. Yanga imetangaza hatua tano itazochukua kufuatia kufuatia hukumu iliyotolewa Agosti 2, 2023 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kutotambulika kwa Baraza la Wadhamini la klabu hiyo
Hukumu hiyo, imeitaka bodi iliyokuwa madarakani kwa katiba ya mwaka 1968 iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2011, kurudi madarakani kuongoza klabu ya Yanga.
Baraza linalolamikiwa linaongozwa na Mwenyekiti George Mkuchika na wajumbe wake Mama Fatma Karume, Dk Mwigulu Nchemba, Tarimba Abbas na Antony Mavunde.
Mkurugenzi wa sheria wa Yanga, Patrick Saimon alisema kuwa wamebaini mapungufu mengi katika kesi iliyopelekea uamuzi wa kutotambulika kwa Baraza lao hivyo baada ya hapo watachukua hatua nne.
“Cha kwanza, jopo la wanasheria wa klabu ya Yanga wameshapeleka maombi mahakamani kuomba kuongezewa muda wa kufanya mapitio ya kesi.
“Jambo la pili ambalo tutafanya, klabu itapeleka maombi ya kufanywa mapitio upya ya kesi kwa sababu hao waliofanya hawakuwa na uhalali wa kufanya hivyo.
“Cha tatu klabu ambacho itafanya itapeleka maombi ya kuzuia utekelezaji wa hii hukumu ambayo wameiomba mahakama ya Kisutu iwasaidie kuondoa uongozi mzima wa klabu ya Yanga.
“Jambo la nne ambalo klabu imefanya tayari tumeshawasiliana na mama yetu, kipenzi chetu Wanayanga, Mama Fatma Karume na Mzee wetu Jabir Katundu ili kusudi waweze kushirikiana na uongozi waweze kufungua kesi ya jinai kwa kughushi saini zao,” alisema Patrick.
Wakili Patrick amesema kuwa baada ya hapo, wahusika wote waliofungua kesi hiyo dhidi ya klabu, watapelekwa kwenye mkutano mkuu ili wanachama waamue nini cha kuwafanya.
Alisema kuwa wameamua kufanya hivyo kwa sababu suala hilo ni la kisheria na hasa ukizingatia kuwa muda wa kufanya marejeo na kukata rufaa umekwisha bila ya wao kuwa na taarifa kutokana na ukweli kuwa uongozi haukuwa na wito wa mahakama.
Amefafanua kuwa wameamua kufanya mambo hayo matano kutokana na hujuma zilizopo dhidi ya klabu yao kwani pia wamegundua kuwa Juma Ally, Geofrey Mwaipopo na Abeid Mohamed Abeid siyo wanachama halali wa klabu hiyo.
“Baada ya kupata hukumu, tuliomba Makahama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kufanya upekuzi wa kasi na kugundua mambo kadhaa ikliwa pamoja na ujanja ujanja ambao uliokuwa unatumika.
Kwanza, wito wakuitwa mahakamani ulikuwa unapokelewa na Abeid Mohamed Abeid ambaye alijtambulisha kuwa anawawakilisha wadhamini wengine na klabu kwa ujumla. Abeid alikuwa anakubali kila hoja iliyokuwa inatolewa mahakamani dhidi ya uongozi wa klabu,” alisema Patrick.
Kesi hiyo ilifunguliwa Agosti 4, 2022 ambapo walalamikaji walipinga kutambuliwa kwa Bodi ya Wadhamini ya Yanga, ambayo ilianzishwa chini ya katiba ya mwaka 2010, wakitaja upungufu wa kisheria.
Katika hukumu yake, mahakama iliamuru Bodi ya Wadhamini ya Yanga, chini ya katiba ya mwaka 1968 iliyorekebishwa mwaka 2011, irejee kwenye majukumu yake ya kusimamia na kuendesha shughuli za klabu hiyo.
Zaidi, mahakama pia iliamua kuwa Bodi ya Wadhamini chini ya katiba ya mwaka 1968 iliyorekebishwa mwaka 2011 inapaswa kuandaa, kuitisha, na kuwezesha mkutano wa wanachama wa klabu kwa madhumuni ya kuchagua wanachama wapya wa Bodi ya Wadhamini.
Kwa upande wake, msajili wa klabu na vyama vya michezo, Evordy Kyando alisema kuwa hana taarifa rasmi kuhusiana na hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu dhidi ya uongozi wa Yanga.
Kyando alisema kuwa yeye amekuwa akifuatilia sakata hilo kupitia vyombo vya habari. “Siwezi kuzungumzia suala hilo kutokana na ukweli kuwa halipo rasmi kwangu, mimi pia nasoma na nasikiliza kupitia vyombo vya habari.
Nitaangalia kwenye mafaili yangu kujua undani wake, kwa sasa sina jibu kamili kuhusiana na sakata hilo,” alisema Kyando.
Kwa upande wake, msemaji wa msemaji wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi, (RITA) Jafari Malema hakuweza kuzungumzia suala hilo huku akitoa maelekezo kwa huduma ya kupata taarifa za masuala ya ufafanuzi utolewa kwa kuandika barua na kuomba upekuza wa taarifa za wadhamini ambapo utalipia.
“Pia unaweza kwenda kwenye club husika kuomba kupatiwa status ya wadhamini waliopo kwa sasa fika ofisini RITA makao makuu, utakutana na wahusika. Kwa sasa nipo mkoani kikazi,” alisema Malema.
Juhudi za kuwasaka wanachama hao waliofungua kesi hiyo ziligonga mwamba kutokana na simu zao kutopokelewa na licha ya kutumiwa ujumbe wa simu haukujibiwa.