Sakata la Yanga, TFF bado ngoma ngumu
Muktasari:
- Yanga imeingia katika sintofahamu ya TFF ambapo Benki ya CRDB na wenyewe wameingilia kati sakata hilo.
Dar es Salaam. Klabu ya Yanga imeendelea kulikomalia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhusu zawadi yao ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano Mei 11, 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu, Andre Mtine alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoka TFF.
"Sisi hatutaki chochote zaidi ya zawadi yetu ya ubingwa kama kuna jambo lolote watuwasilishie kwa njia ya maandishi ila kwa sasa hatuhitaji jambo lolote zaidi ya zawadi yetu ya ubingwa," amesema Mtine.
Sakata hilo la madai ya fedha za ubingwa ziliibuliwa na Yanga ambao walidai haitocheza mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida Black Stars msimu huu hadi itakapolipwa fedha za zawadi za msimu uliopita.
Juzi Jumatatu, Juni 9, 2025, Ofisa Habari wa Yanga, Ałły Kamwe alisema kuwa wanajiandaa kutocheza mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwa vile hawajapewa fedha zao za zawadi ya ubingwa za msimu uliopita.
“Taarifa hii iwafikie ofisi ya Katibu Mkuu wa TFF na wadhamini wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB kuwa hatutacheza mchezo wa Fainali wa CRDB siku ya tarehe 28 mpaka tutakapolipwa hela yetu ya ubingwa kwa msimu uliopita. Tumevumilia dharau hizi kutoka kwa mamlaka za soka kwa muda mrefu sana. Sasa imefika mwisho. Hii ya Zanzibar pia hatutacheza,” alisema Ałły Kamwe.
Siku moja baada ya Yanga kutoa taarifa hiyo kuwa haitocheza mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Singida Black Stars msimu huu hadi itakapolipwa fedha za zawadi za msimu uliopita, Benki ya CRDB inayodhamini mashindano leo ilitoa ufafanuzi na kujiweka kando na suala hilo.
Benki hiyo ilisema kuwa ilishafanya malipo ya fedha hizo kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
“Benki ya CRDB inapenda kutoa ufanunuzi wa madai yaliyotolewa na Msemaji wa Klabu ya Yanga katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika tarehe 09 Juni 2025 katika Makao Makuu ya klabu hiyo.
“Katika mkutano huo, Msemaji wa Klabu hiyo alinukuliwa akitoa taarifa kwa Shirikisho la Mpira wa Migu Tanzania (TFF) na kwetu kama Mdhamini Mkuu wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB kuwa Klabu ya Yanga haitocheza fainali za mashindano hayo msimu huu kama hawatolipwa fedha za ubingwa wa msimu uliopita.
“Tungependa kufahamisha umma na wadau wote wa soka kuwa Benki ya CRDB ni taasisi yenye kuzingatia weledi, kanuni na taratibu
na kwa msingi huo tayari Benki ilikwisha tekeleza kikamilifu wajibu wake wa kifedha kwa TFF kama sehemu ya makubaliano ya udhamini wa mashindano haya. Malipo yote ya msimu uliopita yalifanyika kwa TFF kwa mujibu wa mkataba baina ya Benki ya CRDB na TFF.
Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo akizungumza na waandishi wa habari, leo Jumatano Juni 11, 2025 baada ya Yanga kuleta barua ya madai yao. Picha na Michael Matemanga
“Benki ya CRDB inatambua kuwa mbali na mchezo wa soka kuunganisha jamii yetu na kutoa burudani, lakini pia mchezo huu ni ajira kwa vijana wengi, hivyo dhamira yetu ni kuendelea kushirikiana na TFF, vilabu na wadau wengine katika kukuza mchezo huu kwa maslahi mapana ya Taifa letu,” ilifafanua taarifa hiyo ya CRBD.
Chanzo cha madai hayo ya Yanga ni msimamo wake wa kutocheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Simba, Juni 15, mwaka huu hadi mambo manne inayohitaji yatakapofanyiwa kazi.
Mambo hayo manne ni kuvunjwa kwa kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi, kuwepo kwa Bodi huru ya Ligi, kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa TFF na kujiuzulu kwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania.