Samatta kucheza na kina Pogba, Dembele Ufaransa
Muktasari:
- Mbwana Samatta amewahi kuzichezea Simba, TP Mazembe, KRC Genk, Aston Villa, Fenerbahce, Royal Antwerp na PAOK kabla ya kujiunga na Le Havre.
Paul Pogba, Takumi Minamino, Bree Embolo, Andrew Ayew, Mohammed Salisu, Olivier Giroud, Ousmane Dembele, Marquinho, Vitinha na Khvicha Kvaratskhelia ni baadhi ya nyita ambao nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta atakutana nao katika Ligi Kuu ya Ufaransa 'Ligue One' msimu ujao.
Samatta ataonekana katika Ligi Kuu ya Ufaransa 'Le Havre' baada ya leo, Agosti 5, 2025 kujiunga rasmi na Le Havre kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea PAOK ya Ugiriki
"Ally Samatta ni wingu na maji. Rekodi ya ina yake yenye sifa zilizoandaliwa vizuri. Ally Samatta mshambuliaji mwenye uzoefu amejiunga rasmi na Le Havre AC.
"Ndani ya Tanzania kuna alama mbili za kitaifa: Mlima Kilimanjaro na Ally Samatta. Na ilivyo sio vigumu kwa HAC kusogeza milima, ilikuwa rahisi kumleta kiongozi wa Taifa Stars, jina la utani la timu ya taifa ya Tanzania," imefafanua sehemu ya utambulisho wa Samatta uliofanywa na Le Havre.
Samatta anajiunga na Le Havre akiwa mchezaji huru kwani alimaliza mkataba wake na PAOK baada ya msimu uliopita kumalizika na anaandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligue One.
Mshambuliaji huyo ametua Le Havre baada ya timu hiyo ya Ufaransa kukoshwa na kile ambacho mshambuliaji huyo amekionyesha msimu uliopita akiwa na kikosi cha PAOK.
Licha ya siku za mwanzo za msimu uliopita kuonekana kuwa ngumu kwa Samatta kutokana na kutopata nafasi ya kutosha ya kucheza, mshambuliaji huyo alimaliza msimu vyema akifunga mabao matano katika mechi 20 huku akipiga pasi tatu za mwisho.
Kabla ya hapo, Samatta amecheza kwa mafanikio katika klabu mbalimbali zinazoshiriki Ligi tofauti duniani ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia kumfanya awe na uzoefu mkubwa wa soka la ushindani.
Jina la Samatta lilianza kuvuma zaidi wakati alipokuwa akiitumikia TP Mazembe ambayo akiwa anaichezea, timu hiyo ilitwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya DR Congo pamoja na taji moja la Ligi ya Mabingwa Afrika huku akishinda tuzo ya mfungaji bora na pia mwaka 2015 aliibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora Afrika kwa Ligi za Ndani.
Baada ya hapo alijiunga na KRC Genk ambayo alishinda nayo taji la Ligi Kuu ya Ubelgiji kisha baadaye akazitumikia Aston Villa, Fenerbahce, Royal Antwerp na PAOK.
Ndani ya Le Havre, Samatta atavaa jezi namba 70.