Samatta, Mwalimu waitwa Taifa Stars
Dar es Salaam. Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kimetangazwa rasmi, jana, Jumapili na kocha Hemed Suleiman 'Morocco' kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya michezo miwili ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Congo Brazzaville na Niger.
Stars ambayo iliishia robo fainali katika michuano ya CHAN ambayo ilifanyika kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki, itaanza kambi hiyo Septemba 2, 2025 (kesho, Jumanne), ikiwa na nyota 23 huku wachezaji wanne tu wakiwa ndio wanaocheza soka la kulipwa nje.
Katika kikosi hicho, nyota wa muda mrefu Mbwana Samatta (Le Havre AC, Ufaransa), Saimon Msuva (Al-Talaba SC, Iraq) wapo kuhakikisha safu ya ushambuliaji inabaki na makali yake.
Pia, chipukizi Antony Remmy kutoka Azam FC U20 amepewa nafasi ya kujumuika na wenzake, jambo ambalo linaashiria mkakati wa kujenga kizazi kipya cha wachezaji wa Stars.
“Tunapaswa kuandaa timu yenye uwiano wa uzoefu na vipaji vipya. Hii siyo safari fupi, ni mwendelezo wa maandalizi ya kuhakikisha tunakuwa na kikosi chenye ushindani kila eneo. Vijana wapya watapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wakongwe kama Samatta na Msuva,” alisema Kocha Hemed.
Safu ya ulinzi inaendelea kuwa na wachezaji waliothibitisha ubora wao kwa muda mrefu kama vile Shomari Kapombe (Simba), Mohamed Hussein, Dickson Job, Ibrahim Hamad 'Bacca' wote kutoka Yanga.
Katika eneo la kiungo, majina kama Mudathir Yahya, Feisal Salum na Yahya Zaid yamejumuishwa, huku Kocha Hemed akibainisha wamejitahidi kufanya machaguo ya wachezaji kulinga na mipango ya mechi hizo.
"Tumekuwa tukiangalia wachezaji ambao wanaweza kutusaidia kulingana na mpango wa mechi ambazo zipo mbele yetu," alisema.
Katika kikosi hicho pia amejumuishwa mshambuliaji hatari wa Clement Mzize ambaye alifunga mabao mawili katika mashindano ya CHAN.
Kwa mujibu wa benchi la ufundi, Stars itaingia kambini mapema ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa na muda mzuri wa kuzoeana na kuimarisha mbinu za uchezaji. Mechi hizo mbili dhidi ya Congo Brazzaville na Niger zinatarajiwa kuwa na umuhimu mkubwa katika mstari wa Tanzania kufuzu kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia.
Taifa Stars inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi E sawa na Niger ambayo ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi sita, kundi hilo linaongozwa na Morocco yenye pointi 15.
Kikosi kamili kilichoitwa: Makipa, Yakoub Suleiman (JKT Tanzania), Hussein Masaranga (Singida BS) na Antony Remmy (Azam FC U20).
Mabeki ni Shomari Kapombe (Simba), Luseajo Mwaikenda (Azam), Wilson Nangu (JKT Tanzania), Mohamed Hussein (Yanga), Pascal Msindo (Azam), Ibrahim Abdulla (Yanga) na Dickson Job (Yanga).
Viungo ni Yusuph Kagoma (Simba), Novatus Dismas (Göztepe FC, Uturuki), Yahya Zaid (Azam), Malta), Mudathir Yahya (Yanga), Feisal Salum (Azam)
Washambuliaji ni Edmund John (Yanga), Charles M’Mombwa (Floriana FC, Clement Mzize (Yanga), Abdul Hamis (Azam), Mbwana Samatta (Le Havre AC, Ufaransa), Saimon Msuva (Al-Talaba SC, Iraq), Iddy Selemani (Azam na Selemani Mwalimu (Simba).