Senzo: Siendi Simba, Azam mimi ni Yanga

Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingiza.

WANACHAMA na mashabiki wa Yanga wamepata mshtuko mkubwa baada ya kupata taarifa juzi usiku juu ya Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Masingisa kugoma kuongeza mkataba, lakini mwenyewe amevunja ukimya na kufunga kila kitu, ikiwamo ishu ya nyota aliyerejea Yanga, Bernard Morrison.

Uongozi wa Yanga ulitoa taarifa usiku wa juzi ikimshukuru Senzo kwa utumishi wake uliotukuka klabuni hapo miaka miwili iliyopita na kufanya mitandaoni mjadala kwa wadau wa soka hususani wanayanga ni juu ya kitendo cha kigogo huyo kuachana na Yanga kuanzia rasmi leo Agosti Mosi.

Hata hivyo, Mwanaspoti lilimsaka Senzo na kufanya mahojiano maalumu ambapo aliweka bayana kwamba kuondoka kwake Jangwani, wala sio kwa jambo baya kama wadau wengi wanavyovumisha mtandaoni na kusisitiza kuondoka ni mipango yake ya maisha nje ya Tanzania.

Senzo, aliwashusha presha mashabiki wa Yanga akiwaambia kwamba kamwe hawezi kurejea Simba kwa sasa wala kufanya kazi klabu nyingine ikiwamo Azam na kwamba atafanya kazi nje ya Tanzania huku akiongeza yeye ni mwanachama wa klabu hiyo.

“Ni uamuzi wangu kwa mustakabali wa maisha yangu, hakuna kibaya chochote kinachoniondoa hapa Yanga, hii ni familia yangu nami ni mwananchi hili naomba watu walielewe rasmi kutoka kwangu,” alisema Senzo na kuongeza;

“Nimeona watu wananiuliza kama narejea Simba au nakwenda Azam niwambie hapana sitakwenda huko nakwenda kufanya kazi zangu nje ya Tanzania, mimi ni mwanachama wa Yanga na nina kadi ya uanachama na nimefurahi sana kufanya kazi hapa nchini.”

Aliongeza ana imani kubwa na uongozi wa Rais Mpya wa Yanga, Injinia Hersi Said na kwamba uongozi huo utafanya makubwa ndani ya klabu hiyo na yuko tayari kuwashauri wakati wowote.

“Hersi (Said) ni rafiki na kaka yangu pamoja na Arafat (Haji) na wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji, bahati mbaya naondoka wakati sijafanya nao kazi lakini wote nimekuwa nikishikiana nao vizuri ndani na nje ya klabu,” alisema Senzo aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba na kuongeza;

“Naamini mambo yatakuwa mazuri zaidi katika utawala huu,wananchi wenzangu wawape viongozi ushirikiano, nawashukuru serikali ya Tanzania, mamlaka ya vibali vya kazi, shirikisho la soka, Bodi ya Ligi na wote niliyoshirikiana nao hapa, naamini kila mmoja alifurahia jinsi tulivyoshirikiana.”

Kuhusu kupishana kwake mara mbili na kiungo mshambuliaji, Bernard Morrison, Senzo alisema wala hana tatizo na usajili wa nyota huyo kutoka Ghana na kwamba alihusika mara zote kumsajili ndani ya klabu hizo kubwa nchini za Simba na Yanga.

“Niliwahi kuwaambia ninyi Mwanaspoti juu ya Morrison, bahati mbaya hapa Tanzania uongo hupewa nafasi kubwa kusambaa, nilisema nilipokuwa Simba nilihusika kumleta Morrison pale, ila wakati anafika nilikuwa naondoka klabuni hapo,” alisema Senzo na kuongeza;

“Nilipokuwa Yanga pia imekuwa hivyohivyo, viongozi wenzangu wanajua jinsi tulivyoshirikiana kumleta huyu Morrison, ni mchezaji bora bila kuangalia mambo yake yanayosemwa, nina imani kubwa atakwenda kuwafanyia kazi kubwa wananchi ambao wamempokea tena bila kinyongo, hata mimi nitafarijika nikisikia Morrison akiwa anafanya kazi bora hapa.”

“Unajua hata wakati nakuja hapa Yanga natokea Simba, wako ambao waliniona mpuuzi naacha klabu nzuri nakwenda timu isiyokuwa na rekodi ya kuchukua mataji wala uongozi bora, ila nilikuwa na uhakika nakwenda kuungana na familia salama na sasa wanaona juhudi ya kazi yetu,”