Serikali ya Tanzania yaanika rushwa kwenye soka nchini

Tuesday May 04 2021
serikalipic

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Deo Ndejembi akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha bunge la bajeti jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

By Habel Chidawali

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema inatambua uwepo kwa vitendo vya rushwa katika mchezo wa soka vinavyoikosesha mapato.

Hayo yameelezwa leo Mei 4, 2021 bungeni mjini Dodoma na naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya ya Rais Utumishi na Utawala Bora,  Deo Ndejembi na kubainisha kuwa Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inakumbana na vitendo hivyo kwa kufanya uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya viingilio katika mechi mbalimbali.

Katika swali la msingi mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi alihoji ni kwa kiasi gani Serikali inakabiliana na kudhibiti vitendo vya rushwa katika michezo.

Katika majibu yake Ndejembi amesema matokeo ya uchambuzi huwezesha kubaini na kuziba mianya ya rushwa kwenye eneo hilo na mapato huongezeka.

Ametolea mfano kuwa katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa Machi 2019, mapato yaliongezeka hadi kufikia Sh206 milioni kwa watu 50,233 waliokata tiketi ukilinganisha na mapato ya  Sh122 milioni kwa watu 47,499 waliokata tiketi kwa mechi iliyochezwa Januari 2019 kwenye uwanja huo.

"Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya michezo nchini, mwaka 2016 Takukuru iliunda timu maalum ya uchunguzi kufuatilia na kuchunguza vitendo vya rushwa katika michezo ambapo kesi tatu zimefunguliwa mahakamani na tuhuma saba zinaendelea kuchunguzwa," amesema Ndejembi.

Advertisement

Amewataka viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wasimamizi wa soka na viwanja vya michezo waruhusu na kushirikiana na Takukuru kuweka matangazo ya kukemea rushwa kwenye soka na michezo kwa ujumla.

Advertisement