Simba Bingwa ASFC 2020/21

SIMBA wameibuka kuwa mabingwa wa kombe la Azam (ASFC) kwa msimu huu baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Yanga kwenye mechi ya fainali iliyopigwa jioni ya leo Julai 25  kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Hii ni kwa mara ya pili mfululizo kwa Simba kubeba ubingwa huo kwani walifanya hivyo msimu uliopita kwa kuwafunga Namungo kwenye mchezo wa fainali iliyopigwa uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.

Hilo lijakuwa kombe la tatu kwa Simba msimu huu baada ya kubeba lile la Simba Super Cup, la Ligi Kuu Tanzania Bara na hili la ASFC.


MCHEZO ULIVYOKUWA

Kipindi cha kwanza kipimalizika kwa suluhu (0-0) huku Yanga wakiwa pungufu baada ya kiungo Tunombe Mukoko kuoneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea faulo Nahodha wa Simba John Bocco.

Pia kwa upande wa Simba Clatous Chama alioneshwa kadi ya njano baada ya kuonekana akijibizana na mwaamuzi kwa kufoka.

Kipindi cha pili kilirejea kwa Yanga kurudisha timu nyuma na kushambulia kwa kushitukiza wakati watani zao Simba wakifunguka na kutafuta mabao.

Dakika ya 58 Joash Onyango wa Simba alioneshwa kadi ya njano baada ya kumsukuma Yacouba Songne wa Yanga katikati ya uwanja.

Simba walifanya mabadiliko dakika 68 kwa kumtoa Rally Bwalya na nafasi yake kuchukuliwa na Benard Morrison na Yanga kujibu mapigo dakika ya 75 kwa kuimuingiza Fiston Abdoul kuchukua nafasi ya Yacouba.

Yanga walifanya mabadiliko mengine dakika dakika ya 77 kwa kumtoa Ditram Nchimbi na kuingia Fareed Mussa.

Dakika ya 79 Taddeo Lwanga aliwafungia Simba bao la kwanza na la pekee katika mchezo huo baada ya kumalizia kwa kichwa kona iliyopigwa na Jose Miquissone na kuoneshwa kadi ya njano kwa kuvua flana wakati wa kushangilia.

Muda huo jukwaa la Simba lilinyanyuka kwa shangwe huku lile la Yanga likipoa na katika jukwaa la pamoja linalotenganishwa na mlango wa kuingilia, mashabiki wa timu zote mbili walionekana wakirushiana chupa za maji.

Baada ya bao hilo Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Chama na nafasi yake kuchukuliwa na Erasto Nyoni na dakika tatu baadae Yanga wakamtoa Tuisila Kisinda na kuingia Deus Kaseke.

Dakika ya 90 Simba walimtoa Chriss Mugalu na nafasi yake kuchukuliwa na Kennedy Juma aliyeingia kumalizia mchezo kwani sekunde chache mbele mechi ilimalizika Zawadi Mauya wa Yanga akioneshwa kadi ya njano sekunde za mwisho mwisho.

Pamoja na kufunga, pia kiungo wa Simba Lwanga ndiye aliibuka mchezaji bora wa mechi hiyo ya fainali.