Simba hesabu mbili kwa Azam

Friday December 31 2021
kocha PIC
By Charles Abel

Benchi la ufundi la Simba limewaahidi mambo mawili mashabiki wake wakati watakapokabiliana na Azam FC kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1 usiku.

Kocha wa Simba, Pablo Franco amesema kuwa wamejiandaa kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo lakini pia kucheza soka safi litakalowapa burudani.

“Kwetu imekuwa wiki nzuri mandalizi yameenda vyema na kila mmoja yuko tayari kwa majukumu yaliyo mbele yake. Tunakutana na timu ngumu na bora yenye wachezaji wazuri, imebadilisha kocha na imekuwa ikifunga mabao.

Jambo la msingi tunatakiwa kuendana na ubora wetu. Wachezaji wamenionyesha kuwa wanataka kuichezea timu hii na wana malengo. Nafahamu Azam FC itakosa wachezaji watatu tegemeo ambao wameenda kuichezea Zimbabwe lakini naamini wana wachezaji mbadala wa kucheza katika nafasi zao,” alisema Pablo.

Kocha huyo alisema kuwa hawana wanachokihitaji zaidi ya ushindi kesho.

“Ni kweli tumekuwa tukifanya vizuri dhidi ya Azam lakini historia haiwezi kutupa ushindi ingawa tumejiandaa kupata matokeo mazuri.

Advertisement

Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutusapoti kama ambavyo wamekuwa wakifanya. Tumejiandaa kupata ushindi na kucheza soka zuri na la kuvutia,” alisema Pablo

Advertisement