Simba kuanza kusajili wanachama wapya, viongozi wasema…
Muktasari:
- Vuguvugu la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Simba lilianza Julai 2016 wakati mfanyabiashara Mohammed Dewji alipotangaza nia ya kutaka kuwekeza kwenye klabu ya Simba kwa kiwango cha hisa cha asilimia 50 alizotangaza atazinunua kwa kiasi cha Sh20 bilioni.
Dar es Saalam. Baada ya kukaa kwa miaka saba bila kufanya usajili wa wanachama wapya, Simba imetangaza kufufua mchakato huo hivi karibuni, ikitamba kwamba itaongoza kwa kusajili idadi kubwa zaidi Tanzania.
Mara ya mwisho kwa Simba kuendesha zoezi hilo ilikuwa ni 2018 na baada ya hapo haikulifanya tena.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 19, 2025 amesema kuwa usajili wa wanachama ni hatua za mwanzo za kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.
"Mchakato wetu wa mabadiliko ambao tulianza 2017 unaenda kufikia tamati ni kipindi kigumu tumepitia maana huu mfumo unatumika ulaya hasa ujerumani ila Afrika hakuna Klabu inayotumia, tuliona ugumu ambao mamlaka za serikali na Wizara zilivyopata changamoto kupitisha
"Kubwa ambalo tunaenda kulifanya, tulikuwa tumesimamisha usajili wa wanachama lakini sasa tunaenda kutoa kadi za wanachama. Tunaenda kuwa klabu ya kwanza yenye wanachama wengi, sio tu Tanzania. Na wanachama ambao wanakuja kuwa wanahisa. Sasa tunaenda kufanya mambo makubwa," amesema Magori.
Katika hatua nyingine, Magori amesema kuwa uongozi wa Klabu hiyo uko imara na hakuna migogoro baina yao kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa.
"Sisi tuna bahati tumepata mwekezaji ambaye kwanza ni mwanachama wa Simba. Kwa hayo maneno maneno tunayaua na tunakuwa kitu kimoja. Lugha za kutugawanya tunaomba zifike mwisho, Simba ni moja. Tunaenda kutengeneza timu ya kisasa ambayo ina utawala bora. Tusikubali kuyumbishwa," amesema Magori.
Vuguvugu la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Simba lilianza Julai 2016 wakati mfanyabiashara Mohammed Dewji alipotangaza nia ya kutaka kuwekeza kwenye klabu ya Simba kwa kiwango cha hisa cha asilimia 50 alizotangaza atazinunua kwa kiasi cha Sh20 bilioni.
“Shabaha yangu ni kuitoa klabu kwenye Bajeti ya Bilioni 1.2 hadi Bilioni 5.5. Mashabiki wa Simba wanahitaji mafanikio ya haraka. Lazima tusajili vizuri na tuajiri makocha wazuri. Ukitenga Bilioni 4 kwa mwaka, tayari umewazidi wapinzani Azam na Yanga," alinukuliwa Mfanyabiashara huyo.
Suala hilo la Dewji liliibua vuguvugu ndani ya klabu hiyo ambapo lilikuja kusababisha kubadilishwa kwa katiba yake na kupatikana mpya ambayo inabariki mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na kuifanya Simba iwe Kampuni huku mfanyabiashara huyo akishinda zabuni ya kuwa mwekezaji kwa asilimia 49 ya hisa za klabu hiyo.
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, amekanusha taarifa zinazosambaa kuhusu kuwepo kwa mgogoro kati ya uongozi wa klabu hiyo na mwekezaji wake, akisisitiza kuwa mahusiano baina yao ni mazuri na mawasiliano yanaendelea kwa uwazi.
Akizungumza kuhusu mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’, Mangungu amesema mawasiliano yao ni ya karibu, akieleza kuwa mara ya mwisho walizungumza ni jana saa nane, hatua inayodhihirisha kuwa hakuna mpasuko kama inavyodaiwa.