Simba kushusha mafundi watatu wapya

Muktasari:

  • Juma Mgunda amesaini mkataba wa mwaka mmoja Simba na klabu hiyo iko kwenye mchakato wa kuajiri makocha watatu kwa mpigo, Mwanaspoti limeambiwa.

Juma Mgunda amesaini mkataba wa mwaka mmoja Simba na klabu hiyo iko kwenye mchakato wa kuajiri makocha watatu kwa mpigo, Mwanaspoti limeambiwa.

Makocha hao ni wa viungo, makipa na bosi wa Mgunda ambaye taarifa za ndani ya klabu hiyo zinaeleza kwamba majukumu yake yatabadilika mara baada ya ujio wa kocha mkuu.

Mbali na Mgunda, pia klabu hiyo imempa Mohammed Muharami ‘Shilton’ mkataba wa muda mfupi wa kuwa kocha wa makipa wakati mchakato wa kupata kocha wa nafasi hiyo ukiendelea.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema mchakato wa kupata kocha mkuu unakwenda sanjari na wa kupata kocha wa makipa na kocha wa viungo.

“Bado mchakato ni mbichi kabisa, kama nilivyosema wanaotuma maombi wengi ni wa nchi za Ulaya, Afrika bado hakuna aliyeomba, klabu hiko kwenye hatua za awali kabisa za kupitia CV za waliokwisha tuma maombi,” alisema.

Kuhusu Mgunda na Shilton kupewa mikataba, Ahmed alisema tayari makocha hao wanamikataba, lakini watabaki kuwa makocha wa muda kwenye nafasi zao za sasa hadi pale mchakato wa kupata makocha wapya utakapokamilika.

“Wote wawili wana kaimu nafasi hizo, ni makocha wa muda, wakati mchakato wa kupata makocha ukiendelea, watakapopatikana basi klabu itajua nini cha kufanya kwao,” alisema Ahmed.

Ingawa gazeti hili linafahamu kwamba Mgunda amesaini mkataba wa mwaka mmoja mwanzoni mwa wiki hii wenye kipengele cha kuwa kocha msaidizi mara baada ya kocha mkuu kupatikana.

Mgunda ambaye ameiongoza Simba katika mechi tatu za mashindano na kushinda zote, huku Simba ikicheza bila kuruhusu bao na kufunga matano kwenye mechi hizo ameoekana kukubalika kwa baadhi ya mashabiki wa timu hiyo ambao baadhi yao wanatamani apewe mkataba jumla.

“Anaruhusiwa kuomba, ndiyo sababu mchakato unafanyika, akiomba na viongozi wakaridhia wakampitisha, basi atakuwa kocha mkuu, lakini kwa sasa anakaimu nafasi hiyo hadi pale atakapopatikana kocha mkuu,’’ alisema Ahmed.

Mgunda nyota wa zamani wa timu ya taifa juzi alienda nyumbani kwake Tanga kwa mapumziko mafupi kabla ya kurejea kuendelea kuinoa timu hiyo kwaajili ya mechi zijazo.

Mgunda ataendelea kuhudumu Simba kama kocha mkuu kwenye mechi mbili zijazo za mtoano za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi Agosto ya Angola, kabla ya klabu hiyo kupata kocha mkuu.