Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba walivyotumia dakika 40 Jangwani

Paredi la Simba likiwa nje ya Makao Makuu ya Yanga Jangwani, Dar es Salaam.

Dar e salaam. Dakika 40 tu zimetosha kubadilisha hali ya hewa ya Jangwani jijini Dar es Salaam, baada ya Simba kufanya paredi la kusherehekea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB ambapo msafara wao ulipita katika eneo hilo huku mashabiki wakijazana kwa wingi kushuhudia mabingwa hao.

Msafara huo uliwasili Jangwani majira ya saa 8:40 mchana, ukiwa umeambatana na maelfu ya mashabiki waliokuwa wamefurika barabarani, wakisubiri kuipokea timu baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam kwenye fainali iliyochezwa kisiwani Pemba.

Shughuli zilianza kwa mabasi mawili mapya aina ya Iriza kupita kwa mwendo wa taratibu ambapo mashabiki walizunguka msafara huo huku wakishangilia, kuimba na kurusha vijembe kwa wapinzani wao wa jadi waliokuwa na ofisi zao katika eneo hilo.

Baadhi ya mashabiki walionekana wakifuta vioo vya mabasi hayo mapya kama ishara ya furaha na mapenzi kwa klabu yao huku wakati huohuo wakiligeukia gari la Yanga aina ya Yutong lililokuwa limeegeshwa pembeni ya eneo hilo na kulishusha thamani kwa vijembe.

Baada ya kupita kwa mabasi hayo, gari dogo la kifahari lililobeba viongozi wa klabu akiwemo msemaji Ahmed Ally pamoja na nahodha Shomary Kapombe liliwasili katika eneo hilo likiwa limefunguka juu.

Kapombe alionekana akilishika Kombe la CRDB na kulinyanyua juu mara 40 kuonyesha ushindi huo kwa mashabiki.

Mashabiki wa Yanga na Simba wakitambiana wakati wa paredi la Simba likipita nje ya Makao Makuu ya Yanga Jangwani, Dar es Salaam.

Huku Ahmed naye akionyesha Kombe la Muungano ambalo Simba ilitwaa Aprili 2026 baada ya kuifunga Yanga.

Katika kile kilichoonekana kuongeza joto la tukio hilo, wawili hao walitumia muda wao kusimama kwa dakika 13 mbele ya jengo la Yanga ambapo walinyanyua makombe hayo huku mashabiki wakishangilia kwa nguvu na kuendelea kuimba nyimbo za klabu yao.

Baadaye, Ahmed alichukua kipaza sauti na kuendelea kuwasalimia mashabiki huku akiwatupia maneno ya utani wapinzani wao, hali iliyozidi kuongeza shamrashamra katika eneo hilo lililokuwa limefurika.

Matukio hayo yaliambatana na moshi wa rangi ya bluu uliotanda angani, ukizidi kupamba mandhari ya sherehe hizo kabla ya saa 9:00 alasiri msafara kuendelea kuelekea Msimbazi na baadaye kukamilisha kilele chake katika fukwe za Coco.

Licha ya msongamano mkubwa na muda mfupi wa kusimama, Jangwani iligeuka kuwa kitovu cha shamrashamra, ikiwa ni sehemu ya kile ambacho mashabiki walikiona kama siku ya kihistoria ya kurejesha fahari ya Simba baada ya kutwaa ubingwa huo ilioukosa kwa miaka minne mfululizo.