Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yamrejesha Sowah, yampeleka timu ya vijana

Muktasari:

  • Sowah alisimamishwa mapema mwaka huu wakati timu ilipokuwa Dodoma ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara mwezi Februari kabla ya mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Dar es Salaam. Uongozi wa Simba SC umemrejesha mshambuliaji wake raia wa Ghana, Jonathan Sowah, lakini kwa sharti kwamba afanye mazoezi na timu ya vijana ya klabu hiyo chini ya umri wa miaka 20 (Simba U20).

Sowah alisimamishwa mapema mwaka huu wakati timu ilipokuwa Dodoma ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara mwezi Februari kabla ya mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Katika kipindi hicho, alirudishwa Dar es Salaam na tangu wakati huo hajacheza mechi yoyote ya ligi au mashindano.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amethibitisha kuwa mchezaji huyo alifika mbele ya kamati ya nidhamu ya klabu na kupatikana na hatia kwa baadhi ya makosa yaliyokuwa yakimkabili.

Ally alieleza kuwa kamati hiyo imeamua Sowah afanye mazoezi na timu ya vijana chini ya uangalizi wa karibu.

Kurudi kwake kwenye kikosi cha wakubwa kutategemea mwenendo wake na kama kamati itaridhika na maendeleo yake.

“Kwa sasa, Sowah bado ni mchezaji wetu na anatakiwa kufanya mazoezi na timu ya U20.

“Hii ni sehemu ya mchakato wa kumfuatilia, na pindi kamati itakaporidhika na tabia yake, atarejea kwenye kikosi cha wakubwa,” amesema Ally.

Awali, Sowah alisisitiza kuwa bado ana mkataba na Simba na akaeleza mapenzi yake kwa klabu hiyo licha ya changamoto za kinidhamu.

Aliongeza kuwa soka ni taaluma yake na anaendelea kujitoa kwa Simba, akifichua kuwa aliwahi kukataa ofa ya kucheza katika ligi kuu ya Afrika Kusini ili kujiunga na klabu hiyo.

“Ninaipenda Simba, ndiyo maana nilichagua kujiunga nayo na nikakataa ofa kutoka Afrika Kusini. Soka ni kazi yangu na itaendelea kuwa kazi yangu siku zote,” alisema Sowah.