Simba, Yanga sasa zinachuana hapa

Wednesday August 04 2021
mchezajipic
By Charity James

SIMBA na Yanga zinachuana kuwania saini ya beki wa kati wa Biashara ambaye alikuwa anawaniwa Azam FC, Abdulmajid Mangalo, aliyefanya vyema msimu ulioisha kama nahodha.

Habari za uhakika kutoka mmoja wa wasimamizi wa mchezaji huyo ni kwamba Simba na Yanga mpaka jana jioni wote walishampa mikataba lakini alikuwa hajasaini na yote alikuwa akitembea nayo kwenye gari bila klabu hizo kujijua.

Ingawa inaelezwa kwamba mwenyewe alikuwa anakaribia kusiani Simba juzi jioni, ila upepo uligeuka baada ya watu wa Yanga kumuendea hewani na kuonyesha nia ya kumsajili. “Anaangalia ni wapi penye masilahi zaidi lakini kidogo tu asaini Simba wikiendi, baadaye ndio akashauriwa kusubiri kwanza aangalie upepo, lakini ana mkataba wa Simba na Yanga yote anatembea nayo kwenye gari na lolote linaweza kutokea muda wowote.

Vigogo wa Simba walimkatia tiketi ya ndege Mangalo ambapo aliingia Dar es Salaam Ijumaa usiku na jana alionekana katikati ya Jiji la Dar es Salaam akipiga misele na wasaidizi wake. Habari zinasema Simba wanamsainisha Mangalo kutokana na umri wake mdogo wakijua watamtumia muda mrefu kwenye nafasi ya ulinzi sambamba na wakongwe Wawa na Onyango.

Alipoulizwa Mangalo alisema yuko kwenye mazungumzo ya usajili Jijini Dar es Salaam lakini; “Kwasasa sina nafasi ya kuzungumzia hilo, kwani ukweli utajulikana muda si mrefu, tuvute subra tu, kama ni Simba au Yanga nikishakamilisha nitawajulisha.”

Biashara jana walikuwa wakirushiana mpira juu ya hatma yake lakini kuna kila dalili kwamba wamempa baraka atimke.

Advertisement
Advertisement