Simba yatoa ufafanuzi jezi mpya za Caf

Muktasari:
- Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema sababu za kibiashara ndizo zimepelekea waamue kuanza kuuza jezi zao mpya za hatua ya makundi kuanzia Februari 15 badala ya muda mfupi baada ya kuzizindua juzi kama wengi walivyotegemea.
SIMBA juzi usiku ilizindua uzi mpya wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutangaza kuwa jezi hizo zingeanza kuuzwa Februari 15, lakini mabosi wa klabu hiyo wametoa ufafanuzi wa kauli hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema sababu za kibiashara ndizo zimepelekea waamue kuanza kuuza jezi zao mpya za hatua ya makundi kuanzia Februari 15 badala ya muda mfupi baada ya kuzizindua kama wengi walivyotegemea.
"Siku hizi tunafanya kitu kulingana na matakwa ya soko. Hilo ndilo kubwa kuliko kitu chochote. Ukiweza kujua soko lako linataka nini na ukitengeneza kulingana na soko umefanya umefanya vizuri. Timu inarudi Feb 12 baada ya mechi ya Guinea. Huwezi kuuza timu ikiwa haipo. Timu iwepo ndio uuze," alisema Kajula na kuongeza;
"Kupanga ni kuchagua. Kumbuka hii mechi ya kwanza tunaanza kucheza nje halafu tunakuja ndani. ni mkakati mzuri kujenga kuelekea mechi kubwa, uuzaji wa jezi unakuwa sehemunya mkakati wako."
Kajula alisema wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo wa kwanza dhidi ya Horoya wakiamini itawaweka katika nafasi nzuri ya kupata ushidni katika mchezo utakaofuata nyumbani dhidi ya Raja Casablanca, itakayopigwa Februari 18.
Simba imeibuka kivingine katika hatua hiyo ya Ligi ya Mabingwa kwa kuweka nembo ya Visit Tanzania kwa ajili ya kutangaza utalii wa nchi kutokana na mdhamini wao mkuu, kampuni ya ubashiri wa matokeo ya michezo ya M-Bet kuwa na mgongano wa kimaslahi na miongoni mwa wadhamini wa mashindano yaliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).
Kwa mujibu wa Kajula, timu hiyo haitopata chochote kupitia mkataba huo zaidi ya kuunga mkono juhudi za serikali kutangaza utalii.
"Tanzania ni nyumbani kwa asilimia 50 ya Simba wote duniani, kimantiki hiyo Simba haijakosea kuwa Tanzania. Lakini upande wa pili utalii ndio unachangia pato la fedha za kigeni Tanzania. Timu yetu ya wanaume ipo katika timu 10 bora Afrika, timu ya wanawake ni ya nne Afrika na tukiwa na mitandao yenye nguvu Afrika, Tanzania tunaongoza."
"Maana yake tunaweza kutangaza Tanzania na nje ya Tanzania. Simba ikitangaza Tanzania itaongeza pato la Taifa," alisema Kajula.
Simba imefikia uamuzi wa kutumia nembo ya Visit Tanzania baada ya makubaliano na mdhamini wao mkuu M-Bet.
"Tukisafiri tutakuwa na M-Bet, siku moja kabla ya mechi na siku ya mechi ndio tutakuwa tunatumia Visit Tanzania kama ilivyo matakwa ya CAF,"Ahmed Ally.
Mkurugemzi wa masoko wa M-Bet Tanzania, Allen Mushi alisema hawana kipingamizi kwa timu hiyo kutumia nembo hiyo ambayo inautangaza utalii wa nchi nje ya mipaka yake.
“Kampuni ya M-Bet ni wazalendo na baada ya kupokea ombi la Simba, hatukuwa na kipingamizi kwani kupitia mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simva inakwenda kuitangaza nchi kupitia vivutio vya utalii na hivyo kuongeza pato la taifa,” alisema Mushi.