Simba yatupwa nje FA

Muktasari:

  • Simba iliendelea kuruhusu bao la mapema baada ya kufungwa dakika ya 5 kwa kichwa, mfungaji akiwa mshambuliaji Reliant Lusajo akimalizia mpira uliopalazwa na kichwa cha beki Che Malone Fondoh kufuatia mpira wa kona iliyopigwa na beki, Mpoki Mwakinyuke.

Simba imelitema taji la pili ndani ya siku nne baada ya jana kuishia hatua ya 16 bora ya Kombe la FA, iking'olewa na Mashujaa kwa matuta 6-5.


Simba iliendelea kuruhusu bao la mapema baada ya kufungwa dakika ya 5 kwa kichwa, mfungaji akiwa mshambuliaji Reliant Lusajo akimalizia mpira uliopalazwa na kichwa cha beki Che Malone Fondoh kufuatia mpira wa kona iliyopigwa na beki, Mpoki Mwakinyuke.


Mashujaa mpaka wanapata bao hilo, ilionekana kuwa na kasi ya kutengeneza mashambulizi kuelekea lango la Simba na kufanikiwa kufunga bao la kuongoza.


Dakika za nyongeza kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza, Mashujaa walipata pigo baada ya beki na nahodha wao, Said Juma Makapu kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu baada ya awali kupewa kadi ya kwanza ya njano alipomchezea vibaya kiungo Clatous Chama, kisha dakika chache baadaye kumkwatua Said Ntibazonkiza na mwamuzi Hans Mabena kumtoa nje.


Kipindi cha pili, Mashujaa ilirudi na mpango wa kucheza kwa tahadhari ikikaa nyuma kulinda bao lao, hatua ambayo iliwaruhusu Simba kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ambapo dakika ya 50 alikuwa mshambuliaji Freddy Michael aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Pa Omar Jobe kuisawazishia timu yake akipokea pasi ya Kibu Denis.


Simba iliishambulia zaidi Mashujaa, lakini umakini wa washambuliaji na viungo wake ulikuwa mdogo kuweza kutengeneza mabao zaidi ambapo mpaka dakika 90 zinakamilika, timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1, ndipo hatua ya penalti ikachukua nafasi yake.


Mashujaa ilirudia tena historia kwa kuwang'oa Simba baada ya kufanikiwa kupata penalti 6 zilizofungwa na Samson Madeleke, Michael Masinda, Idrisa Stambuli, Adam Adam, Mpoki Mwakinyike na Baraka Mtui, huku penalti yao iliyopaishwa ilipigwa na Zuber Dabi.


Simba wao penalti zao tano zilifungwa na Mohamed Hussein 'Tshabalala', Israel Mwenda, Fredy, Mzamiru Yassin na Ladack Chasambi, huku waliokosa ni Willy Onana na Sadio Kanoute ambapo kipa Erick Johora zote alizidaka na kuwa shujaa wa Mashujaa.