Simu ya Pablo yamleta winga

Tuesday December 28 2021
simupic
By Thobias Sebastian

WAKATI mabosi wa Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez wakitarajiwa kukutana leo jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali ikiwamo ishu za usajili, winga Harrison Mwendwa anajiandaa kutua nchini baada ya kupigiwa simu na Kocha Mkuu wa watetezi hao wa Ligi Kuu Bara, Pablo Franco.

Winga huyo Mkenya anayekipiga kwa sasa Kabwe Warriors ya Zambia, ni mmoja wa nyota wawili wa kigeni ambao wapo kwenye rada za Simba na wanatajiwa kuja nchini kusaini mikataba yao na kukinukisha kupitia michuano ya Kombe la Mapinduzi 2022 inayoanza Januari 2, mjini Unguja.

Mwendwa aliliambia Mwanaspoti kwa mara ya kwanza kuwa amewasiliana na Kocha wa Simba na kumueleza wazi ni miongoni mwa wachezaji anaowahitaji katika dirisha hili dogo la usajili.

Winga huyo aliyewahi kuja hapa nchini akiwa na Kariobangi Sharks katika michuano SportPesa Super Cup, alisema Pablo alimpigia simu kumuulizia ishu ya mkataba wake na kama yupo tayari kuja Simba kwenye dirisha dogo kwa maelezo amevutiwa na uchezaji wake kwani amemfuatilia.

Alisema baada ya mazungumzo hayo alimjibu Pablo kuwa yupo tayari kuja kucheza Simba ambayo ilifanya jaribio la kutaka kumsajili mwaka 2018, ila walishindwana kwenye masilahi.

“Najiandaa kuja Simba siku sio nyingi, ili kuja kumalizana katika mazungumzo ya kimkataba, Pablo amesema ananitaka na viongozi wa klabu hiyo wamewasiliana na wakala wangu kwa muda tofauti. Kama mambo yakienda vizuri nitasaini na kuwa mchezaji mpya wa klabu hiyo kubwa Afrika,” alisema Mwendwa na kuongeza;

Advertisement

“Nikifika Simba baada ya kumalizana nao kama Pablo alivyonieleza mwenyewe ndio atafanya uamuzi nicheze mechi za Ligi Kuu Bara au nianzie kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, niliyojulishwa inaanza mapema mwakani.”

Winga-teleza huyo aliongeza kwa kusema; “Bado nina mkataba wa mwaka mmoja na nusu hapa Kabwe walionichukua baada ya kuichezea AFC Leopards kwa muda mfupi, ila Simba wanafahamu yote haya na mpaka nimefanya uamuzi wa kuja huko Tanzania kwa ajili yao lazima watafuata taratibu za usajili ikiwemo klabu yangu ya Kabwe kufahamu kila kitu.

“Simba ni timu kubwa yenye wachezaji wazuri, Wakala wangu amenifahamisha hilo kwani upande wake aliongea na viongozi wa Simba kuona jinsi gani watanipata, kwahiyo hapa nawasubiri tu wao wafuate taratibu pamoja na kutuma tiketi kutoka huku Zambia nipo tayari kuja Tanzania kwa ajili yao.”

Mwaka 2018, Simba walimtaka Mwendwa baada ya kufanya vizuri kwenye Kombe la SportPesa ila walishindwa kumpata kama ilivyokuwa kwa Yanga walioonyesha nia ya kumhitaji baada ya klabu yake ya wakati huo Kariobangi Sharks kutaja dau la Dola 50,000 (zaidi ya Sh100 milioni).

Simba ili kumpata Mwendwa wakati huu kutoka Kabwe inatakiwa kulipa Dola 25,000 zaidi ya Sh50 milioni kuvunja mkataba wake na baada ya hapo ndio watakubaliana na mchezaji pesa ya usajili pamoja na mshahara atakaovuta kila mwisho wa mwezi.


MABOSI WAITANA

Mabosi wa Simba leo wanatarajiwa kukutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ikiwamo ishu za usajili na maandalizi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na ile ya Mapinduzi watakayoshiriki mapema mwakani.

Kwa mujibu wa tarifa kutoka Simba ni kwamba kikao hicho kitajumuisha Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Try Again, Mtendaji Mkuu, Barbara na Kamati ya Usajili ya klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Kassim Dewji na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Mabosi hao wanakutana kujadili usajili wa nyota wanaotakiwa na kocha wao kwa ushiriki wa mechi zao za ndani na zile za kimataifa, huku mezani kwao kuna majina ya Mwendwa, Alex Bazo, Clatous Chama na wachezaji wawili wazawa akiwamo kipa Metacha Mnata anayewaniwa pia na Yanga ambayo ilimtema mwishoni mwa msimu uliopita.

Advertisement