Singida BS vs Yanga mwisho wa ubishi

Kiporo cha mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) 2022-2023 kitaliwa leo kwenye Uwanja wa Liti (zamani Namfua), uliopo mjini Singida.

Kiporo hicho kinazikutanisha Yanga inayotetea taji hilo ililolitwaa msimu uliopita na Singida Big Stars inayocheza hatua hiyo kwa mara ya kwanza ikiwa ndio kwana imepanda Ligi Kuu Bara msimu huu ikitoka Ligi ya Championship ikitumia jina la DTB.

Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa kuanzia saa 9:30 alasiri  baada ya kukwama kuchezwa Mei 7 mwaka huu kutokana na Yanga kuwa na majukumu ya mechi za kimataifa.

Pambano hili linazikutanisha timu hizo, huku Yanga ikiwa imetoka kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuing'oa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, lakini ikiwa tayari ni bingwa wa Ligi Kuu ikitwaa mapema kabla haijamalizia kwani imeswaliwa na mechi za raundi mbili.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana kwenye michuano hiyo, lakini litakuwa ni pambano la tatu kwa timu hizo kukutana msimu huu, kwani tayari zilishacheza mechi mbili za Ligi Kuu na mara zote Yanga imeibuka na ushindi.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Novemba 17, mwaka jana Yanga ilishinda jijini Dar es Salaam kwa mabao 4-1 na waliporudiana Mei 4 Singida ikiwa nyumbani ilikubali kichapo kingine cha 2-0.


MECHI YA KIBABE

Licha ya Singida kupoteza mechi mbili mfululizo za ligi msimu huu mbele ya Yanga, lakini bado haichukuliwi poa kutokana na rekodi tamu na uzoefu mkubwa alionao kocha wa timu hiyo, Hans Pluijm aliyewahi kuiongoza Yanga kubeba ubingwa 2015-2016 na kuifikisha fainali Singida United.

Kocha huyo Mhalanzi aliifikisha Singida fainali ya michuano hiyo ya ASFC mksimu wa 2017-2018, japo ilipoteza kwa mabao 3-1 mbele ya Mtibwa Sugar waliobeba taji kwenye fainali kali iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Baadhi ya mastaa wa timu hiyo akiwamo Meddie Kagere, Amissi Tambwe, Said Ndemla, Pascal Wawa ni wazoefu wakubwa wa michuano hiyo kwani wamewahi kutwaa mataji ya ASFC wakiwa na Simba na Yanga, hivyo wanajua ugumu wa pambano hilo la nusu fainali.

Kubwa zaidi ni kwamba licha ya Singida kujihakikishia kumaliza ndani ya Nne Bora ya Ligi Kuu na kukata tiketi ya michuano ya kimataifa msimu ujao, ikiungana na Yanga, Simba na Azam, bado haitaki kumaliza msimu kinyonge kwa kutaka kutinga fainali na hata kubeba taji kabisa mwezi ujao.

Mshindi wa pambano hilo atatinga fainali na kuungana na Azam iliyotangulia mapema kwa kuing'oa Simba kwa mabao 2-1 katika nusu fainali kali iliyopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Tayari kocha Hans na baadhi ya mastaa wa timu hiyo wametamba kwamba wanataka heshima ya kuitungua Yanga na kwenda fainali kibabe kabla ya kumaliziana na Azam ambao iliyowahi kutwaa taji hilo msimu wa 2018-2019.


YANGA NA REKODI ZAKE

Kama hujui hii itakuwa ni nusu fainali ya saba kwa Yanga kati ya misimu nane mfululizo wa michuano hiyo ikiwa ni rekodi ya aina yake kwa wababe hao wa soka la Tanzania.

Ni msimu mmoja tu wa 2017-2018 ndio Yanga ilishindwa kuingia nusu fainali baada ya kutolewa mapema, lakini misimu mingine iliyosalia tangu michuano hiyo iliporejeshwa tena mwaka 2015 baada ya kusimama kwa muda mrefu wakati ilipokuwa ikifahamika kama michuano ya Kombe la FA 2002.

Katika msimu wa kwanza wa kurejeshwa kwa michuano hiyo enzi za utawala wa Jamal Malinzi ndani ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), Yanga ilicheza nusu fainali na Coastal Union katika mechi iliyojaa vurugu za kupigwa kwa marefa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Licha ya vurugu hizo, Yanga ilishinda mabao 2-1 na kutinga fainali na kukutana na Azam FC ilioyokuwa imetoka kuitoa Mwadui kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya 2-2. Yanga ilishinda fainali hiyo na kubeba ubingwa kwa kuifumua Azam kwa mabao 3-1.

Msimu uliofuata wa 2016-2017, Yanga ilishiriki kama mtetezi na kutinga nusu fainali kwa kuvaana na Mbao FC jijini Mwanza na kutolewa nishai kwa kufungwa bao 1-0 na kulitema taji baada ya beki wa kati enzi hizo, Andrew Vincent 'Dante' kuchomesha na safari ya wana Jangwani ilikwamia hapo.

Mbao ilienda fainali jijini Dodoma kuvaana na Simba iliyokuwa imetoka kuifumua Azam kwa bao 1-0 na Mnyama kubeba taji kwa mbinde mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa kwa muda wa dakika 120.


YATOKA KAPA, YARUDI UPYA

Msimu wa 2017-2018 Yanga ilitoka kapa baada ya kutolewa mapema na kuikosa kwa mara ya mechi ya nusu fainali na msimu huo taji lilibebwa na Mtibwa Sugar iliyoifumua Singida United kwa mabao 3-2 mechi iliyopigwa jijini Arusha.

Yanga ilienda kujiuliza na kujipanga upya kabla ya kurudi na moto msimu wa nne wa michuano hiyo kwa kutinga nusu fainali ya msimu huo wa 2018-2019, lakini ikatibuliwa na Lipuli iliyowatungua kwa mabao 2-0. Lipuli ilienda fainali kuivaa Azam iliyoitoa KMC kwa bao 1-0 na Wanapaluhengo hao ikicheza Uwanja wa Samora, mjini Iringa ilipigwa 1-0 na Azam kubeba taji hilo la kwanza la ASFC.

Yanga iliendelea kuonyesha umahiri wake wa kutinga nusu fainali kwani msimu wa 2019-2020 ilifuzu tena na kukutana na watani wao, Simba na kujikuta ikipta aibu kwa kufumuliwa mabao 4-1 kwenye pambano lililokuwa la upande mmoja na Simba kutinga fainali ikienda kucheza na Namungo.

Namungo iliyokuwa imepanda Ligi Kuu msimu huo, ilifuzu fainali kwa kuifunga Sahare All Stars ya Tanga katika pambano kali lililopigwa, Mkwakwani Tanga na Simba iklishinda taji kwa mabao 2-1 mechi iliyopigwa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Mabingwa hao wa kihistoria wa michuano hiyo na Ligi Kuu Bara, waliendeleza moto tena kwenye ASFC kwa msimu wa 2020-2021 ilipotinga tena nusu fainali na kukutana na Biashara United ambao iliwachapa bao 1-0 na kufuzu fainali kuumana na Simba ilitoitungua Azam pia kwa bao 1-0.

Fainali ya mechi ya msimu huo ilipelekwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma na Simba kuifumua Yanga kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na kiungo mkabaji, Taddeo Lwanga ikiwa ni kipigo cha pili mfululizo kwa Vijana wa Jangwani mbele ya Mnyama kwenye michuano hiyo.

Msimu uliopita, Yanga ilikomaa tena na kutinga nusu fainali na safari hii ilikutana  na watani wao, Simba na mchezo ukapelekwa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Tofauti na mechi za misimu miwili iliyopita ya michuano hiyo safari hii Yanga ilikomaa na kuvua joho la unyonge kwa kuifumua Simba kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na kiungo mshambuliaji, Feisal Salum 'Fei Toto' kwa shuti kali na kuivusha timu hiyo kwenda fainali jijini Arusha.

Katika mechi hiyo ya fainali, Yanga ilivaana na Coastal Union iliyokuwa imeitoa Azam kwa penalti 6-5 baada ya dakika 90 kuisha kwa suluhu na pambano hilo lililopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid lilimaliza dakika 120 kwa sare ya 3-3 kabla ya Yanga kuibuka mabingwa kwa ushindi wa penalti 4-1.


YANGA AU SINGIDA?

Kwa msimu huu Yanga ilitinga nusu fainali zake za saba kwa kuifunga Geita Gold kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam. Bao la Fiston Mayele ndilo lililoivusha Yanga hatua hiyo na kesho Jumapili itakuwa na kazi ya kupambana kuvuka ili iende fainali.

Timu hiyo inakutana na Singida ambayo ilifika hatua hiyo kwa kuifumua Mbeya City kwa mabao 4-1 katika mechi ya robo fainali.

Hivyo bila ya shaka mchezo wa kesho utamaliza ubishi na tambo za timu hizo katika kuzitumia dakika 90 ili kuifuata Azam inayowasubiri kwa hamu kwa pambano la fainali litakalopigwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga katikati ya Juni mwaka huu.

Je, ni Yanga itakayofuzu ili iendee kutetea taji kwa Azam au ni Singida inayowatibuliwa wana fainali hao wa michuano ya CAF na kwenda kuandika rekodi ya kubeba taji la msimu huu? Tusibiri tuone!