Siri ya Mwanaspoti kudumu miaka 20

Muktasari:

  • Leo ni siku ya pekee. Mwanaspoti tumetimiza miaka 20 tangu tuingie mitaani mwaka 2001.

Leo ni siku ya pekee. Mwanaspoti tumetimiza miaka 20 tangu tuingie mitaani mwaka 2001. Ni safari ndefu iliyopitia changamoto mbalimbali, lakini tumeweza kuipita na kwa mafanikio makubwa kutokana na kusimamia weledi, kusikiliza maoni ya wasomaji na kutoa habari za uhakika tumefika siku ya leo. Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu (pichani) anasema katika kipindi hicho cha miaka 20 gazeti hili limekuwa kioo cha habari za michezo na burudani nchini Tanzania na Kenya ambako kote linachapishwa na kuuzwa.

“Tumepita katika vipindi mbalimbali vya mabadiliko, Mwanaspoti ililazimika kubadilika kimuundo, kimuonekano pamoja hata na staili ya uandishi ili kuendana na hali halisi na ndio maana kitakwimu mpaka sasa tumebaki kuwa ndio gazeti lenye mamlaka zaidi kwenye mambo ya michezo nchini,” anasema Machumu.

“Ndio gazeti ambalo linasomwa sana kwa vile lina mambo mbalimbali ndani yake ambayo yanagusa kada zote na michezo yote.”

Machumu ambaye amefanya kazi MCL kwa takribani miaka 17 mfululizo, anasema katika kipindi hicho ameshuhudia mabadiliko mengi ambayo yalilenga kukidhi matakwa ya wasomaji wa gazeti hili.

“Kipindi cha nyuma wigo wetu wa habari ulikuwa mdogo, lakini kadri miaka ilivyokuwa ikienda tukazidi kuboresha na kubadilika, na mahitaji ya walaji au wasomaji wetu yakaongezeka zaidi tukaanzisha toleo la Kenya ambalo kwa sasa linafanya vizuri nchini humo, ndio gazeti la Kiswahili linafanya vizuri zaidi nchini humo… hiyo yote ni kutokana na umahiri wetu.

“Kuchapishwa na kuuzwa kwa Mwanaspoti kunalifanya kuwa gazeti kubwa kabisa la michezo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Hakika tunajivunia mafanikio haya ya bidhaa ya Tanzania kupeperusha bendera ya nchi yetu juu katika sekta ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.

“Lakini pia Mwanaspoti la sasa lina habari za takwimu zaidi, uchunguzi, ripoti maalumu, uchambuzi wa wataalamu mbalimbali kwenye matoleo yetu kama kina Edo Kumwembe, Mwalimu Kashasha, Ezekiel Kamwaga, Ally Mayay na wengine wengi ambao lengo la kuwaweka ni kutaka kuwapa wasomaji vitu vilivyochambuliwa kwa kina.

“Yaani wapate majibu sahihi ya kile wanachokihitaji kwa wakati muafaka na kutoka kwa watu sahihi,”anasema Machumu huku akisisitiza kwamba waliamua kufanya mabadiliko hayo ili kuendana na kasi iliyopo duniani. Machumu anasema kwamba katika miaka ya hivi karibuni gazeti hili limekuwa likijikita zaidi kwenye uandishi wa kidijitali na uchunguzi ili kumpa msomaji zaidi ya kile alichosikia, kukisoma au kukiona jana yake kwenye mitandao ya kijamii ama anachokifahamu.

“Habari za michezo kwa sasa zipo kwenye mitandao kila mahali na msomaji anaweza kuzipata siku ya pili, kama gazeti lazima kufikiria kitu tofauti na chenye maelezo ya kina,” anasema Machumu ambaye pia ni mhariri mtendaji mkuu wa MCL, na enzi zake za uandishi alijikita zaidi kwenye habari za biashara na uchumi.

“Katika kuzingatia hilo tumetoa mafunzo kwa waandishi wetu ili wawe na uwezo mkubwa wa kuchanganua mambo ya uandishi wa kina wa habari zinazotokea (day two journalism) na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika hilo, ndio maana hata uandishi wao na wa Mwanaspoti lenyewe ni tofauti zaidi na magazeti mengine yaliyopo nchini.”

Machumu anasisitiza kwamba utofauti mwingine unaolifanya Mwanaspoti kuwa tofauti na magazeti mengine ni kutokana na maono na dhima ya kampuni.

“Kwanza dhima ya MCL inasema lazima tuwe wa kwanza kutoa habari za uhakika, pia tunalenga kuelimisha na kuburudisha, na kuwapa habari bora wanamichezo na wadau wetu Afrika Mashariki na duniani kote,” anasema.

“Kwa vile siyo Wakenya tu na Watanzania wanalitegemea Mwanaspoti ni dunia nzima, tupo kwenye mitandao ya kijamii na kila dakika tunatoa taarifa mpya kadri zinavyotokea na tupo kwenye matukio yote muhimu ndani na nje ya nchi.”

Machumu anaongeza kuwa sera ya MCL inachochea uwajibikaji kwa masilahi ya Taifa na inaunga mkono utengamano wa kikanda na jumuiya mbalimbali ambazo Tanzania ni mshirika.

“Mwanaspoti limekuwa likiibua habari nyingi ambazo zimekuwa na mijadala kwa wanamichezo na kutoa pia masuluhisho ya mambo mbalimbali yenye utata yanayotokea michezoni,” anasema.

“Katika kufanya hilo hatubagui michezo, ndio maana kwenye gazeti letu kila siku kuna kurasa mbalimbali zinagusa michezo ya kila aina, hilo limetusaidia zaidi kuaminika kwenye jamii ya wanamichezo nchini.

“Vilevile mwongozo wetu mwingine ni kusimamia sera ya uhariri pamoja na ile ya mitandao ya jamii, sambamba na Kamati ya Kusimamia utekelezaji wake (Editorial Commitee) ambayo inahakikisha weledi unasimamiwa.”

Machumu anasema moja ya changamoto ambazo Mwanaspoti limepitia ni mabadiliko ya kiteknolojia duniani ambapo katika kukabiliana na hilo kumekuwa na kujiimarisha zaidi kwenye dijitali na kuripoti habari mbalimbali kwa haraka na kwa uhakika ambazo kesho yake zimekuwa zikiboreshwa na kutoka zikiwa zimeshibishwa zaidi kwenye gazeti.

“Tumekuja na application inaitwa e-Gazeti ambayo msomaji akiwa popote pale (duniani) anaweza kununua Mwanaspoti na magazeti mengine ya MCL ambayo ni Mwananchi na The Citizen kwa kadri anavyotaka, kwa vile kuna viwango mbalimbali nafuu vya kulipia na kulipata gazeti kwa wakati msomaji akiwa popote pale,”anasema.

“Dunia ya sasa inakwenda kwa ushirikiano (collaborations) ambapo makampuni yanaunganisha uwezo na kutoa huduma bora kwa pamoja. Ni kwa muktadha huo, MCL kwa kushirikiana na kampuni ya Hype interactive - inayoendeshwa na vijana wavumbuzi wa Kitanzania (kama ilivyo kwa wagunduzi wa eGazeti – Dau Technologies) tumeanzisha App ya Mwanaspoti (Soka App) ambayo inakupatia matokeo, habari, video na takwimu za ligi ya hapa nyumbani na nyinginezo.”

Kwa namna ya kipekee kabisa Machumu amewashukuru Wahariri waliowahi kuliongoza Mwanaspoti kwa nyakati tofauti tangu liasisiwe ambao ni Conrad Dastan (marehemu), Charles Mateso, Denis Msacky, Frank Sanga, Joster Mwangulumbi, Abdul Mohammed, Ndaya Kassongo, Rashid Kejo na Joseph Damas na Michael Momburi. Pia anawashukuru wasomaji kwa kuendelea kuliunga mkono Mwanaspoti na anaahidi litazidi kuboreshwa zaidi huku akiahidi kwamba kuna saprazi kubwa inakuja kuanzia wiki ijayo ndani ya Mwanaspoti ambayo itawaongezea uhondo zaidi kwa gharama ileile ya Sh500.

“Ahsanteni sana kwa kutuunga mkono kwa miaka 20. Wakati tukijipanga kujiimarisha kwa miaka mingine mingi ijayo, ni wajibu wetu kuwarudishia fadhila. Kaeni mkao wa kula,” alimalizia Machumu.