SUPASTAA UTAMUELEZA NINI WEWE!

SUPASTAA UTAMUELEZA NINI WEWE!

Muktasari:

UNA ndoto ya kuwa staa? Au ustaa wa siku mbili umeshakufanya uvimbe kichwa na kujiona zaidi mtaani kwako? Basi kama hufahamu kuna wenzako hao ambao tangu watoto wao ni mastaa na wengine kwa zaidi ya miaka 20 sasa ni mastaa tu na wanazidi kushaini. Utawaambia nini!

UNA ndoto ya kuwa staa? Au ustaa wa siku mbili umeshakufanya uvimbe kichwa na kujiona zaidi mtaani kwako? Basi kama hufahamu kuna wenzako hao ambao tangu watoto wao ni mastaa na wengine kwa zaidi ya miaka 20 sasa ni mastaa tu na wanazidi kushaini. Utawaambia nini!

LULU

Elizabeth Michael a.k.a Lulu alianza kuigiza akiwa na miaka mitano mwaka 2000.

Mashabiki walifahamu kipaji chake kupitia kikundi cha sanaa cha Kaole ambako alikuwa pamoja na marehemu Steven Kanumba, Vincent Kigosi, Mwanaidi Suka na wengine na kung’aa katika tamthlia nyingi za runinga ikiwemo Gharika, Taswira, Zizimo, Taswira, Demokrasia, Jahazi, Tufani, Dira na Sayari.

Baadaye alianza kuigiza filamu akiwa bado na umri mdogo, ambapo filamu yake ya kwanza ilikuwa Misukosuko akishirikiana na Jimmy Mponda na ilipofika mwaka 2006 aliigiza filamu iitwayo ‘Wema’ iliyoandaliwa Kampuni ya Game 1st Quality.

Kuanzia hapo akajikita zaidi katika uigizaji filamu huku filamu nyingine alizocheza ni pamoja na Family Tears, Ripple Of Tears, Passion, Dangerous Girl, House Boy, Woman Of Principles, Linah, Dangerous Girl na Hidaya.

Katika mafanikio yake ya kisanaa, Lulu ameweza kuandaa filamu zake mwenyewe ikiwemo Foolish Age, Mapenzi Ya Mungu Ni Noma na sasa anatesa na tamthilia ya Mimi.

Kwa sasa Lulu, 26, ameonekana kufanya zaidi kazi zake za binafsi na hivi karibuni alifunga ndoa mfanyabiashara Francis Ciza maarufu kama Majizo.

Mr Blue

Awali alijulikana kwa jina la Lil Sama, lakini baada ya kuachia kibao chake cha Mr Blue Blue mwaka 2003, alijizolea umaarufu na mafanikio na kujikuta akipachikwa jina la Mr Blue ambalo ndio anatafutia nalo ugali hadi leo.

Kwa sasa Mr Blue, 33, ambaye aliwahi kutamba na vibao kama Mapozi, Raha, Unanimaliza, Watatukubali, Tabasamu, Pesa, Baki Na Mimi na nyingine nyingi kali kwa sasa ana mke na watoto watatu.


Jeniffer

Hanifa Daud ‘Jennifer’ ni mtoto aliyetamba katika filamu za Uncle JJ na This Is It akiwa na marehemu Steven Kanumba.

Akiwa mtoto mdogo aliweza kufikia hatua hadi ya kulipwa si chini ya Sh 2 milioni za Kitanzania kwa kila filamu anayoigiza kiasi ambacho mastaa wengine wakubwa hawajawahi kukifikia.

Jeniffer alijikuta akiwa anapendwa na rika zote kutokana na uwezo mkubwa alioonesha katika filamu hizo za Kanumba alizocheza kama mtoto mwenye akili katika kufanya mambo yake. Hivi sasa Jenifer yupo mwaka wa pili Chuo Kikuu cha

Dar es Salaam.


Patrick

Alifahamika kama Patrick Kanumba, lakini jina lake halisi ni Othman Njaidi, mtoto wa mama staa wa Bongo Movies, Hidaya Njaidi. Patrick alipata umaarufu kupitia Kanumba baada ya kuigiza kaka wa Jenifer katika filamu za Uncle JJ na This Is It.

Kama hujamwona kwa muda mrefu tangu enzi za Kanumba. ukimuona sasa hautaamini. Patrick kwa sasa amerefuka sana na anakiwasha ile mbaya katika tamthilia ya Pazia inayorushwa na DSTV. Ana kipaji cha kipekee.

Aslay

Kipaji cha Aslay Isihaka kipindi hicho akijulikana kama ‘Dogo Aslay kiligunduliwa na kaka yake aitwaye Idd na ndiye aliyemkutanisha na mdau wa muziki kutoka TMK, Said ‘Mkubwa’ Fella, baada ya kumuona akipenda kuimbaimba kila wakati.

Mwaka 2011 alitoka na wimbo wa ‘Nakusemea’ uliofanya vizuri na kuonekana kupendwa zaidi na watoto na kinamama na mwaka uliofuata, yaani 2012 Aslay alirekodi kibao ‘Umbea’ alichomshirikisha Chegge Chigunda, Niwe

Nawe aliouimba na Temba kabla ya kuachia kete nyingine tena iliyojulikana ‘Bado Mdogo’.

Mwishoni mwa mwaka 2013 liliundwa kundi la Yamoto Band kwa kushirikisha pia vijana wengine watatu ambao ni Beka, Maromboso na Enock Bella huku Aslay akiwa kiongozi wao.

Yamoto walibamba kinoma na ngoma kama Nitakupwelepeta, Nisambazie Raha, Cheza kwa Madoido, Niseme, Bora Kijijini, Su waliomshirikisha Ruby na Mama walioimba na msanii wa nyimbo za taarabu Zena.

Yamoto ilipovunjika 2017, Aslay alikuwa wa kwanza kutoka kundi hilo kuachia ngoma zake mwenyewe ambazo zilizidi kumuweka juu katika soko la muziki.

Nyimbo alizoachia ni pamoja na Angekuona, Muhudumu, Baby, Likizo, Rudi na Usitie Doa aliouimba na malkia wa taarabu nchini, Khadija Kopa. Dogo Aslay a.k.a Dingi Mtoto, kwa sasa ana watoto watatu huku kila mmoja akiwa amezaa na mwanamke mwingine.


Dogo Janja

Dogo Janja naye ni kati ya wasanii ambao wamekulia kwenye usanii kwani akiwa na miaka 12 tu alikukutana na msanii Madee na kumchania mistari kwenye gari yake ambapo alimkubali na kumpa nafasi ya kujiunga na Tiptop Connection.

Hii ilitokea Arusha wakati Wanaume Family na Tiptop Connection walipoenda kufanya shoo klabu ya Triple A. Janja hadi leo anamuita Madee Dady.

Nyimbo alizotesa nazo ni pamoja na My Life, Ngarenaro, Kidebe, Banana, Yente na nyingine nyingi.

Janjaro, 26, aliwahi kumuoa Irene Uwoya, ndoa ambayo haikudumu muda mrefu baada ya wazazi wa Uwoya kutoibariki.


Young D

Pamoja na kuwa na umri mdogo, kupitia kipaji chake hicho, Young D amepata umaarufu na kuweza kuisaidia familia yake pale nyumba yao ilipotaka kupigwa mnada.

Akiwa anazungumzia tukio hilo, Young D anasema alifikia hatua hiyo baada ya kuwepo kwa deni lililosababishwa na marehemu baba yao aliyefariki dunia mwaka 2008 akiwa ni mzee mstaafu.

Baba yao aliugua sana kabla ya kufariki ambapo wakati wa kuugua kwake, kwa sababu familia haikua na uwezo ilibidi wachukue mkopo uliofikia milioni nane ili pesa hizo ziwasaidie kwenye matibabu.

Ili kuikoa ilibidi kutumia hadi senti yake ya mwisho kuikomboa nyumba hiyo na kuweza kurudisha furaha kwa mama yake ambaye alikuwa amepoteza matumaini.

Hata hivyo. anakiri kwamba pesa zote alizozilipa ambazo zilikadiriwa kuwa zaidi ya Sh 8 milioni zilitokana na muziki peke yake.