Tambwe hana utani kabisa!

Sunday October 10 2021
tambe pic
By Yohana Challe


LICHA ya kuanza vyema ligi akiwa na kikosi cha DTB FC, Amisi Tambwe amesema Championship ni ligi ngumu kuliko hata Ligi Kuu Bara.

Kinara huyo wa mabao wa Championship aliyefunga mabao manne kwenye ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya African Lyon wiki iliyopita katika Uwanja wa Uhuru, alisema kila timu imeonekana kujiandaa vyema ili kupanda Ligi Kuu Bara.

“Hii ligi ngumu sana maana kila timu inataka kupanda Ligi Kuu na lengo langu kama ilivyo kwa timu ni kuhakikisha msimu ujao tunapanda daraja,” alisema Tambwe.

Nyota huyo raia wa Burundi ana historia tamu kwenye soka la Bongo tangu akiwa na kikosi cha Simba hasa msimu wa 2013/14 alipokuwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 19.

Hakuishia hapa kwani alipotua Yanga msimu wa 2015/16 alibeba tena tuzo ya ufungaji bora kwa mabao 21 na sasa ameanza kusaka ufungaji bora katika Ligi ya Championship.

Hadi sasa kwenye ligi hiyo mfungaji bora mwenye mabao mengi misimu mitatu iliyopita ni Reliants Lusajo aliyemaliza msimu wa 2018/19 akiwa na mabao 15 na kuipandisha Ligi Kuu timu hiyo.

Advertisement

Kwa upande wake, Juma Abdul, beki wa DTB alisema lengo ni kutangaza ubingwa baada ya michezo 15 kupigwa na ili kutengeneza mazingira hayo wanapaswa kufanya kazi ya ziada kama wachezaji.

DTB FC ndio vinara wa ligi hiyo baada ya kuwa na uwiano mzuri wa mabao na wiki hii itakutana na Green Warriors ambayo nayo ilianza vyema ligi kwa ushindi mbele ya Transit Camp.

Advertisement