Tanzania yaweka rekodi Afrika

Muktasari:

  • Tanzania imekuwa nchi pekee Afrika ambayo imeingiza timu mbili kwenye robo fainali Ligi ya Mabingwa msimu zikiwa ni Simba na Yanga.

Dar es Salaam. Simba imetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kibabe baada ya kuichapa Jwaneng Galaxy mabao 6-0 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Simba imekuwa na kiwango bora kila inapocheza kwenye Uwanja wa Mkapa kwa miaka ya hivi karibuni katika mashindano ya kimataifa.

Simba ilitakiwa kupata ushindi ili kufuzu hatua hiyo muhimu na dakika 22 za kwanza ilishaonyesha kuwa inaweza kupata nafasi hiyo baada ya kuongoza kwa mabao 3-0.

Hii ina maana kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee Afrika ambayo imeingiza timu mbili kwenye robo fainali msimu huu baada ya Yanga kufuzu kwa kuichapa CR Beluoizdad mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Mkapa siku chache zilizopita.

Mabao ya Simba yalifungwa na Saido Ntibazonkiza, Clatous Chama, Kibu Denis, Fabrice Ngoma, Chasambi na Pa Omary Jobe.

Hii inamaana Simba imeendeleza ubabe wake wa kufuzu kwa hatua hiyo kwa mara ya nne katika kipindi cha miaka sita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufanya hivyo msimu wa 2018/2019, 2020/2021, 2022/2023 na msimu huu.

Lakini pia Simba imelipa kisasa kwa Jwaneng ambao waliizuia kufuzu kwa hatua katika msimu wa 2021/2022 baada ya kuichapwa mabao 3-1 kwa Mkapa.

Simba imemaliza nafasi ya pili nyuma ya ASEC Mimosas na sasa inasubiri itapangiwa na nani hatua  ya robo fainali siku chache zijazo.