Simba ina kibarua hiki leo kwa Jwaneng Galaxy

Muktasari:

  • Simba inashika nafasi ya pili katika kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi sita.

Dar es Salaam. Simba ina vibarua vitatu vinavyoilazimisha ipate ushindi wakati leo itakapoumana na Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Kibarua cha kwanza ni kile cha kufuzu hatua ya robo fainali ambapo ikishinda itafikisha pointi tisa zitakazoihakikishia nafasi katika robo fainali ikiungana na ASEC Mimosas iliyoongoza kundi B.

Ikifanya hivyo, itakuwa inafuzu hatua hiyo kwa mara ya nne katika kipindi cha miaka sita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufanya hivyo msimu wa 2018/2019, 2020/2021 na msimu uliopita.

Kazi ya pili ni kulipa kisasi cha msimu wa 2021/2022 pale timu hiyo ya Botswana ilipoifanya Simba isitinge hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Jwaneng Galaxy ilipita kwa kunufaika na kanuni ya mabao ya ugenini baada ya mechi mbili baina ya timu hizo kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 kwani Simba ilishinda mabao 2-0 huko Botswana.

Simba inakabiliwa na kibarua cha tatu ambacho ni kuwa mbabe wa jumla dhidi ya Jwaneng Galaxy kutokana na matokeo ya mechi tatu zilizopita baina yao kutotoa mshindi.

Timu hizo zimewahi kukutana mara tatu tofauti katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Jwaneng Galax ikipata ushindi mara moja, Simba ikishinda mechi moja na mechi nyingine moja ikimalizika kwa sare.

Mechi hiyo ya leo, itachezeshwa na Refa Daniel Laryea kutoka Ghana.