TBF: Tuna imani na Kurasini Heat

Tuesday April 06 2021
TBF pc
By Oliver Albert
By Olipa Assa

Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Phares Magesa amesema shirikisho hilo lina matarajio makubwa na wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Kikapu Afrika (BAL), Kurasini Heat.

Msimu mpya wa BAL unatarajiwa kuanza baada ya mechi za fainali za msimu 2019, ambazo ziliahirishwa kutokana na janga la corona na sasa zitachezwa Mei 16 hadi 30 kwenye Uwanja wa The Kigali Arena, nchini Rwanda, zikishirikisha nchi 12.

Nchi zitakazoshiriki ni Algeria, Angola, Cameroon, Misri, Madagascar, Mali, Morocco, Msumbiji, Nigeria, Senegal, Tunisia, na Rwanda.

“Tanzania tulishiriki na kutolewa kwenye raundi ya kwanza, tulipowakilishwa na JKT, msimu ujao timu ya Kurasini Heat itatuwakilisha,” alisema Magesa.

Alibainisha kwamba tofauti na awali, kipindi hiki, mechi za raundi ya kwanza zitachezwa katika vituo viwili, ambavyo ni Rwanda na Senegal.

“Awali kulikuwa na vituo sita, ila msimu ujao vituo vitakuwa viwili na Tanzania tutawakilishwa na Kurasini Heat, ambayo tunaamini itafanya vizuri na kufika mbali zaidi,” alisema.

Advertisement

Alisema ligi ya msimu ujao itafanyika mara baada ya mechi za fainali za msimu wa 2019 kuchezwa kule Kigali.

“Kama nilivyosema, fainali hiyo iliahirishwa kutokana na corona, ingawa pia Mtanzania, Baraka Sadiki ameweka rekodi ya kuwa mfungaji bora hadi sasa, licha ya JKT kuwa iliondoshwa.

“Msimu huu pia hatuna shaka na Kurasini Heat, ni timu yenye wachezaji wazuri, wazoefu na wenye uchu,” alisema Magesa.

Advertisement