Ten Hag atimuliwa Leverkusen baada ya mechi tatu
Muktasari:
- Ten Hag alichukua nafasi hiyo baada ya kukaa miezi saba bila timu tangu alipotimuliwa Manchester United Oktoba mwaka jana.
Leverkusen, Ujerumani. Kocha wa zamani wa Manchester United, Erik ten Hag, ametimuliwa na Bayer Leverkusen baada ya kudumu kwa siku 62 tu kazini, akisimamia michezo miwili ya Bundesliga na mmoja wa Kombe la DFB-Pokal.
Kocha huyo raia wa Uholanzi aliteuliwa Mei mwaka huu kuchukua nafasi ya Xabi Alonso, aliyekwenda Real Madrid.
Baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya timu ya daraja la nne SG kwenye Kombe la DFB-Pokal lakini mwanzo wake kwenye Bundesliga haukuwa mzuri baada ya timu hiyo kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya Hoffenheim, licha ya kuanza kuongoza kupitia bao la beki wa zamani wa Liverpool, Jarell Quansah.
Leverkusen walipoteza alama muhimu tena Jumamosi, wakiruhusu Werder Bremen waliokuwa na wachezaji 10 kurudisha mabao na mchezo kumalizika kwa sare ya 3-3, hali iliyowaacha wakisuasua katika nafasi ya 12 kwenye Bundesliga.
Hali hiyo imewafanya viongozi wa Leverkusen kuamua kumpiga chini kocha huyo wakati Simon Rolfes, Mkurugenzi wa Michezo wa klabu hiyo, akisema: “Uamuzi huu haukuwa rahisi, lakini wiki za karibuni zimeonyesha kwamba kujenga kikosi kipya na mafanikio chini ya utaratibu huu haiwezekani.”
Ten Hag mwenyewe baada ya sare dhidi ya Bremen alilalamika kwamba kikosi chake hakikuwa tayari, baadhi ya wachezaji hawako fiti, na kikosi kwa ujumla kilishindwa kudumu na kasi mwishoni mwa mchezo.
Leverkusen imepoteza nyota wake kadhaa majira haya ya kiangazi wakiwemo Florian Wirtz, Jeremie Frimpong, Jonathan Tah na Granit Xhaka, hali iliyoifanya klabu hiyo kuingia msimu mpya ikiwa dhaifu.
Ten Hag alichukua nafasi hiyo baada ya kusubili kwa miezi saba bila timu tangu alipotimuliwa Manchester United Oktoba mwaka jana, ambako aliwahi kuondoka wakati timu ikiwa nafasi ya 14 kwenye Ligi Kuu ya England baada ya kushinda mechi nne pekee kati ya 14.