This is Simba! Unaikumbuka mechi ilee!

Msimu wa 2018/19 Simba ilikata tiketi ya Ligi ya Mabingwa na kuingia robo fainali ya michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Awali Simba ilikuwa Kundi D pamoja na JS Saoura (Algeria), Al Ahly (Misri) na AS Vita ya DR Congo. Simba na Al Ahly zilifuzu kutoka kundi hilo.

Ni mechi mbili tu zilitikisa wakati huo, Simba na Nkana Red Devils ya raundi ya kwanza kuyatafuta makundi na ile ya Simba na AS Vita kuingia Nane Bora.

Miamba hiyo ya Tanzania ilikuwa lazima ishinde baada ya kufungwa mabao 2-1 mjini Kitwe, Zambia na marudiano Simba ikashinda mabao 3-1.

Ilikuwa mechi ngumu, lakini mabao ya Jonas Mkude (29), Meddie Kagere (45+1) na Clatous Chota Chama dakika ya 89 yaliipeleka Simba makundi.

Safari ya Nkana ilihitimishwa kwa bao la Chama alilofunga kwa kisigino. Simba iliupiga mwingi katika mchezo ule uliokuwa umejaza mashabiki wa timu hiyo kiasi cha kukosa nafasi ya kukanyaga pale kwa Mkapa. Hakukuwa na jinsi zaidi ya Simba kushinda mchezo ule na ndivyo ilivyokuwa na kukata tiketi ya makundi. Simba iliingia makundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.

Kwa kila aliyeshuhudia mpambano huo, atakubaliana nami ilikuwa mechi ya funga kazi kwa kuwa kila timu ilikuwa na kitu inataka isonge mbele. Simba ikatumia vyema uwanja wa nyumbani, ‘Kila Mtu Ashinde Kwao.’

Hakuna aliyekuwa anaamini. Wapo waliosema mpira ule ungemalizika kwa matuta, kwa kuwa kule kwao, Nkana ilishinda 2-1 na hapa Simba ikawa mbele kwa mabao 2-1. Jumla kuu hapa ni 3-3.

Wapo walioanza kutoka uwanjani wakiamini Simba safari imewakuta, sasa mpira ukaanzia kwa Hassan Dilunga alisababisha hali mbaya Nkana.

Dilunga aliitambuka ngome ya Nkana akapiga krosi ndogo ya chinichini ya alama V na kumkuta Chama aliyeuburuza kifundi kwa kisigino na kuujaza kambani. Hoi hoi, vifijo na nderemo vikatawala. Hiyo ilikuwa dakika 89, Simba ikaingia hatua ya makundi.

Simba vs AS Vita

Ilikuwa Januari 19, 2019 Simba ilipigwa mabao 5-0 na AS Vita mchezo wa kwanza wa timu hizo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Stade de Martyrs.

Baada ya mchezo ule, Simba ikapigwa tena mabao 5-0 na Al Ahly na baadaye ikaenda Algiers, Algeria kuifuata JS Saoura ambao walifungwa mabao 2-0.

Simba ilikuwa Kundi D la michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika ilifanya vyema baada ya kushinda mechi zote nyumbani.

Ilianza kwa kuifunga Saoura mbao 3-0, ikailaza Al Ahly 1-0 kabla ya kucheza na AS Vita mchezo wa mwisho na kuwatandika mabao 2-1. Mpambano ule na AS Vita ulikuwa wa aina yake, kwanza Simba inataka ushindi aingia nane bora, lakini AS Vita nayo ilikuwa inataka nane bora. Ilikuwa Machi 16, 2019, Simba inasawazisha bao dakika ya 38 baada yakutanguliwa kufungwa bao la mapema na Vita. Bao la Simba lilifungwa na Mohamed Hussein Zimbwe kabla ya Chama kumaliza mchezo wote.

Simba ikakata tiketi ya Nane Bora. Ilikuwa mechi ngumu iliyojaa ufundi ambayo Ijumaa iliyopita CAF imeirudisha kama mwanzo. Mechi ya mwaka juzi hadi Simba kufuzu, ilisemwa; afe kipa afe beki, Simba lazima ishinde.

CAF yazirudisha tatu

Timu tatu zinapambana tena, safari hii ikiwa ni tofauti, Al Ahly ndiyo watetezi wakati El Merreikh ni mgeni kikosini (Kundi A). Timu ya nne ilikuwa JS Saoura.

Simba na AS Vita zitacheza mchezo wa kwanza kati ya Februari 12 na 13 wakati mechi ya marudiano itapigwa Kwa Mkapa Aprili 2 na 3.

Bado mechi hiyo itakuwa ya kuamua hatma ya Simba kama ilivyokuwa mechi ya Machi 16, 2019 kwa maana ya kwamba, itakuwa mechi ya mwisho Simba kucheza nyumbani.

Kwa kauli ya ‘Kila Mtu Ashinde Kwao#, Simba itaanza nyumbani na Al Ahly Februari 23, ikiwa ni siku 10 tu baada ya kucheza na AS Vita pale Stade des Martyrs Februari 12 na 13.

Mechi ya pili nyumbani kwa Simba itakuwa dhidi ya El Merreikh itakayokuwa ya marudiano baada ya mchezo wa kwanza utakaopigwa katika Jiji la Khartoum, Sudan kati ya Machi 5 na 6. Sasa shughuli nyingine ambayo Simba itacheza kama fainali kuhakikisha inashinda mechi zote tatu za nyumbani, ni dhidi ya AS Vita. Mechi ya mwisho ugenini ni dhidi ya Al Ahly mjini Cairo.

Kumbukumbu ya mchezo wa Machi 16, 2019 itarudi hapa. Kila shabiki wa Simba atataka kuona Simba inafanya jambo lao kwa Mkapa kwa mara ya pili kwa timu ileile kabla ya kutinga robo fainali. Pamoja na kwamba mechi za ugenini hazina nafasi kubwa ya ushindi pamoja na kwamba uwezekano pia upo, uwanja unaosalia pekee ni wa nyumbani.

Simba ilikata tiketi msimu uliopita baada ya timu za AS Vita na JS Saoura kuharibu mechi zao nyumbani. AS Vita ilitoka sare na Al Ahly nyumbani wakati Saoura na Al Ahly zilitoshana nguvu kule Algiers.