TRA yainunua Tabora United, yaibadili jina
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeingia rasmi kwenye tasnia ya michezo baada ya kukamilisha makubaliano ya kuinunua klabu ya Tabora United na kuibadilisha jina kuwa TRA United Sports Club.
Timu hiyo, ambayo inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa itabaki kuwa ya Mkoa wa Tabora, lakini itasimamiwa moja kwa moja na TRA.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 19, 2025, TRA imesema lengo la umiliki huo ni kutoa burudani kwa walipakodi na Watanzania kwa ujumla, huku pia ikitumia timu hiyo kama chombo cha kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari.
“Timu hii itakuwa sehemu ya kutoa elimu kuhusu masuala ya kodi, umuhimu wa kulipa kodi, pamoja na kueneza ujumbe wa uzalendo na uwajibikaji kwa maendeleo ya Taifa,” imeeleza taarifa hiyo.
Mbali na hilo, TRA imesema kupitia michezo itasaidia kukuza ajira na vipaji vya vijana, sambamba na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
Endelea kufuatilia Mwananchi