Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hesabu kali za kujiokoa Ligi Kuu

Muktasari:

  • Kwa Yanga mbali na vita yake ya ubingwa na Simba, lakini inazigusa timu hizi zinazopambana kutoangukia 'play off' kwani ina mechi mbili dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji.

Ile vita ya kupambana kumaliza ligi nje ya mstari wa kucheza mechi za mtoano 'play off' kuepuka kushuka daraja, mtifuano wake unaanza kesho Jumatano ukiwa unazihusu timu tisa kati ya 16 zinazoshiriki ligi hiyo.

Vita hii ni kali zaidi kwani inahusisha timu nyingi tofauti na ile ya ubingwa inayozihusu Yanga inayoongoza kwa pointi 73 sambamba na Simba iliyopo nafasi ya pili na pointi 72.

Kwa Yanga mbali na vita yake ya ubingwa na Simba, lakini inazigusa timu hizi zinazopambana kutoangukia 'play off' kwani ina mechi mbili dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji.

Hadi kufikia Juni 22 baada ya kucheza mechi za raundi ya 30, zitafahamika timu mbili zitakazocheza 'play off' ya kwanza ikizihusisha zenyewe, kisha itakayopoteza, italazimika kwenda kukabiliana na Stand United iliyofanya vizuri pia katika 'play off' ya Ligi ya Championship kwa kuichapa Geita Gold.

Stand United inapambana kurejea Ligi Kuu Bara kwani tangu iliposhuka msimu wa 2018-2019, imeshindwa kuifikia ndoto yao hiyo kwa takribani misimu sita, hii ni nafasi yao muhimu kufanikisha.

Wakati Stand United ikisubiri mpinzani wa kucheza naye katika 'play off' ya kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao 2025-2026, timu tisa zinazopambana kipindi hiki kuepuka kuangukia kwenye mtego huo ni JKT Tanzania (pointi 35), Dodoma Jiji (pointi 34), Mashujaa               (pointi 33), KMC (pointi 33), Coastal Union (pointi 31), Namungo (pointi 31), Pamba Jiji (pointi 30), Tanzania Prisons (pointi 30) na Fountain Gate (pointi 29).

Katika hili, mtihani mgumu zaidi upo kwa timu za Fountain Gate, Tanzania Prisons, Pamba Jiji, Namungo na Coastal Union ambazo zinapaswa kushinda mechi zote mbili zilizobaki kisha kuziombea mabaya zilizopo juu yao  ili zenyewe zibaki salama.

Lakini upande wa JKT Tanzania, kwao hali sio ngumu sana kwani licha ya kukabiliwa na mechi zote za ugenini, inahitaji pointi moja pekee kujiweka salama zaidi bila ya kuangalia matokeo ya timu zingine, hali hiyo ipo pia kwa Dodoma Jiji itakayoanzia nyumbani na kumaliza ugenini ikihitaji pointi mbili, wakati Mashujaa itakayocheza zote nyumbani na KMC ikishuka dimbani ugenini mara mbili, nazo zinahitaji pointi tatu kila moja.

Kwa upande wa KenGold na Kagera Sugar, kwao ni kama msimu umemalizika kwani zimetangulia kushuka daraja moja kwa moja, huku Tabora United ikiwa haina presha yoyote kutokana na pointi 37 ilizonazo hata ikipoteza mechi zote itakazocheza, haziwezi kufikiwa na timu zilizopo nafasi ya 13 na 14 kwenye mstari wa kucheza mechi za mtoano.

Azam iliyopo nafasi ya tatu na Singida Black Stars ya nne, zina uhakika wa kumaliza hapo huku kila moja ikiwa na tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao. Hivyo mechi mbili zilizobaki kwao ni za kulinda heshima, wakati Yanga na Simba ambazo zenyewe ndizo pekee zina mechi tatu kila moja, zote ni za ubingwa.


Mechi za hesabu kali

Kesho Jumatano, mechi zote nane zimepangwa kuanza saa 10:00 jioni ambapo tatu kati ya hizo, zinazikutanisha timu zote zilizopo kwenye mtego wa kuepuka play off.

Mechi moja itazihusisha timu zinazohitaji pointi sita kuanzia sasa ambapo Coastal Union itaikaribisha Fountain Gate kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, nyingine ni ile ya timu zinazohitaji pointi tatu ikishuhudiwa Mashujaa ikiwa mwenyeji wa KMC, wakati vita nyingine ikiwa kwa Pamba Jiji inayohitaji pointi sita, ikiikaribisha JKT Tanzania yenye uhitaji wa pointi moja pekee.

Mechi zingine ni Namungo inyaohitaji pointi sita ikiikaribisha Kagera Sugar iliyoshuka daraja, wakati Dodoma Jiji inayosaka pointi mbili, ni mwenyeji wa Singida Black Stars. Tanzania Prisons nayo inahitaji pointi sita, itakuwa mwenyeji wa Yanga inayosaka ubingwa.

Baada ya hapo, Juni 22, Mashujaa itakuwa mwenyeji wa JKT Tanzania, huku Pamba Jiji ikiikaribisha KMC, wakati Namungo ikicheza na KenGold iliyoshuka daraja.

Tanzania Prisons itaifuata Singida Black Stars, kama ilivyo kwa Dodoma Jiji ikiifuata Yanga. Coastal Union mwenyeji wa Tabora United na Fountain Gate ikiikaribisha Azam.

Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Ismail 'Laizer' alisema mechi mbili za Ligi Kuu Bara zilizosalia ni ngumu kutokana na mahitaji ya wapinzani wao, akizitaja ndizo zinazomnyima usingizi kwa sasa.

"Maandalizi ni mazuri. Kwa sasa ni kuwapiga tu msasa vijana kwa sababu wachezaji ni walewale ambao nilianza nao msimu na nimerudi nimewakuta, hivyo nitawandaa kisaikolojia," alisema.

Naye kiungo wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana, alisema: "kikubwa tu mashabiki waendelee kutuunga mkono ili mechi zilizosalia tukawafurahishe na kumaliza katika nafasi nzuri kwenye msimamo."

Kwa upande wa Kocha wa Coastal Union, Joseph Lazaro, alisema: “Lazima tujue hadi sasa timu nyingi haziko salama, hata sisi tunahitaji ushindi kwenye mechi zilizobaki kuhakikisha tunakuwa salama kubaki Ligi Kuu, hivyo ushindani utakuwa mkali lakini tutahakikisha tunamaliza vizuri kwani mechi zote tutachezea nyumbani.”

Kocha wa Tanzania Prisons, Aman Josiah alisema katika mchezo ujao dhidi ya Yanga, wanachohitaji ni heshima kwa kuwa mechi hiyo ndiyo itakuwa ya mwisho Sokoine, kabla ya kumalizia msimu ugenini dhidi ya Singida Black Stars.

“Tunakutana na timu tofauti ukilinganisha na zile zilizopita, tunajiandaa kushinda na si vinginevyo, dakika 90 ndizo zitatuamulia, hii ndio mechi ya mwisho hapa nyumbani hivyo tunataka furaha,” alitamba kocha huyo.


WANAOPAMBA KUEPUKA PLAY OFF
                                 P    W    D    L    GF    GA    Pts
6. JKT Tanzania     28    8    11    9    27    26    35
7. Dodoma Jiji     28    9    7    12    30    42    34
8. Mashujaa     28    8    9    11    28    32    33
9. KMC         28    9    6    13    24    41    33
10. Coastal Union 28    7    10    11    24    30    31
11. Namungo     28    8    7    13    23    36    31
12. Pamba Jiji     28    7    9    12    20    32    30
13. TZ Prisons     28    8    6    14    23    38    30
14. Fountain Gate 28    8    5    15    30    54    29