Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Treni inavyookoa timu za Tabora

Muktasari:

  • Ni ile safari ya treni ndiyo iliwaokoa Milambo mwaka 1994, kama ambavyo ndugu zao Tabora United walivyookolewa na treni miaka 30 baadaye, yaani 2024.

Tabora United, warina asali kutoka mjini Tabora, wamefanya lile ambacho wengi wameshindwa kukifanya katika soka la nyumbani, kwa takribani miaka mitano sasa.

Ushindi wao wa 3-1 walioupata Novemba pili mwaka huu dhidi ya Yanga dimbani Azam Complex jijiji Dar es Salaam, umeandika historia ya kuwa kipigo kikubwa cha kwanza kwa Yanga tangu Januari 18, 2020.

Siku hiyo Yanga walifungwa 3-0 na Kagera Sugar, kwenye Uwanja wa Uhuru.

Siku tatu baadaye, yaani Januari 18, 2020, Yanga ikafungwa tena 1-0 na Azam FC, na kuifanya klabu hiyo kongwe kufungwa mechi mbili mfululizo la ligi.

Baada ya hapo, Yanga hawakufungwa tena mabao zaidi ya mawili au kufungwa mechi mbili mfululizo, hadi Tabora United walijazia maumivu ya wananchi juu ya kipigo cha 1-0 kutoka Azam FC.

Lakini hata hivyo, ushindi huu ni kwa mchango mkubwa kutoka SGR, reli ya kisasa chini ya rais wa awamu ya sita, Dk Samia Suluhu Hassan.

Tabora United walipotoka kwao Tabora, walisafiri kwa gari hadi Dodoma walipopanda treni na kuja Dar es Salaam.

Wenyewe wanasema usafiri huo uliwasaidia sana kuwaepusha na uchovu, hivyo kuwa timamu kimwili dhidi ya Yanga.

Walichokionesha uwanjani kila mtu anakijua.

Sasa mkasa wa treni kwa Tabora United unakumbushia ule wa timu nyingine iliyotamba miaka ya 1990, kutoka Tabora, Milambo SC.

Timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1990 na mkuu mpya wa mkoa wa Tabora, Dkt. Lawrence Gama (marehemu), na ilipanda daraja 1992 kushiriki ligi ya 1993.

Ilipandia Singida kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya tjmu ya Mto ya Singida, ambayo baadaye ikawa Singida United.

Milambo ikashiriki ligi daraja la kwanza Tanzania bara kuanzia 1993 hadi iliposhuka mwaka 2001.

Mkasa wao wa treni ulikuwa mwaka 1994, wakiwa katika msimu wao wa pili.

Baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa mwaka 1993 na kumaliza katika nafasi ya tatu hadi kufuzu Ligi ya Muungano, Milambo ilifanya vibaya sana msimu uliofuata, 1994.

Hadi mechi tano za mwisho, Milambo ilikuwa na hali mbaya sana, ikiwa katika nafasi ya 14 katika ligi iiliyokuwa na timu 16, timu tatu zilitakiwa kushuka.

Mechi hizo tano zilizobaki zilikuwa dhidi ya Ushirika ya Moshi, Ndovu ya Arusha, Reli ya Morogoro, Simba ya Dar es Salaam na mechi ya mwisho ilikuwa dhidi ya RTC ya Kagera.

Mechi zote hizi zilikuwa za ugenini kasoro mechi dhidi ya RTC Kagera tu, iliyokuwa ya nyumbani kwenye Dimba la Ali Hassan Mwinyi.

Wakaenda Moshi na Arusha wakafungwa zikabaki mechi tatu ngumu.

Hadi hapo ofisi ya mkuu wa mkoa ikakata tamaa na timu, kwamba itashuka daraja.

Serikali ya mkoa ikaona kuisafirisha timu kwenda Dar es Salaam kucheza na Simba, na Morogoro kucheza na Reli ni kupoteza pesa bure kwa sababu lazima itafungwa.

Hivyo ikawapa wachezaji posho zao (shilingi 7,000 kila mmoja) na kuwaruhusu kuendelea na ratiba zao wakitaka wabaki kambini au waende majumbani hadi itakapokuja ratiba ya mechi ya mwisho dhidi ya RTC Kagera (ambayo sasa ndiyo Kagera Sugar).

Wachezaji wakaitisha kikao chao wenyewe na kukubaliana kwamba waende wao kama wao Morogoro na Dar es Salaam kucheza mechi zao.

Wakati ule timu zilikuwa zinagawana sawa mapato ya milangoni kwa hiyo wachezaji wa Milambo walikubaliana waende wakacheze na ule mgao wa timu yao wagawane wao.

Hadi wanamaliza kikao chao ilikuwa tayari saa mbili usiku, na usafiri wa Tabora kwenda Morogoro na Dar es Salaam wakati ule ni treni tu, na lilikuwa linaondoka saa tano usiku walibaki na saa tatu tu.

Kutoka ilipokuwa kambi yao hadi stesheni ya treni ilikuwa mwendo wa kilomita zaidi ya 15 na hakukuwa na gari.

Wakatoka wakikimbia hadi stesheni, wakakuta ndiyo linataka kuondoka wakaingia hivyo hivyo bila tiketi.

Nauli ya Tabora hadi Morogoro wakati ule ilikuwa shilingi 1000, wakachanga pale na kupata 25,000/= yaani wachezaji 25, wakakata tiketi.

Wakiwa ndani ya treni wakakutana na mtu aliyejitambulisha kwao kama mganga wa kienyeji anayeishi Morogoro, akawaahidi kuwafanyia kazi na kuwapa ushindi, halafu watamlipa baada ya hizo mechi wakakubali.

Wakafika Morogoro saa nane mchana na mechi ni saa kumi jioni.

Wakachukua ‘kigesti cha bei rahisi’ na kubadilisha tu na kwenda uwanjani.

Reli Morogoro ilikuwa timu kali sana wakali na mwaka huo walishiriki Kombe la CAF na kukaribia kufika robo fainali, kabla ya kutolewa na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 5-3 (walifungwa 4-1 ugenini na kushinda 2-1 nyumbani).

Itakumbukwa kuwa uongozi wa mkoa ulishaamua timu isiende kucheza hizo mechi hivyo ukatoa taarifa kwenye vyombo vya habari.

Reli walienda uwanjani kama kukamilisha ratiba tu kwa sababu walishaamini kwamba Milambo haitotokea.

Ghafla bin vu, Milambo hawa hapa wakapigwa na mshangao. Mechi ikachezwa na kumalizika kwa sare tasa.

Bahati mbaya hawakupata pesa ya viingilio kwani mashabiki hawakwenda uwanjani kwa sababu walijua kwamba hakutokuwa na mechi.

Ikabaki mechi ya Simba jijini Dar es Salaam, lakini hawana fedha za nauli.

Wakaita basi dogo la Coaster na kumpanga dereva kwamba watamlipa baada ya mechi.

Wakaondoka wao na mganga wao ambaye tayari walishaanza kumuamini kwa kupata sare na Reli.

Wakafika Dar es Salaam wakiwa hawana hela kabisa, wakachukua ‘kijigesti’ Manzese na kushinda hapo bila kula.

Siku iliyofuata ndiyo ilikuwa ya mechi, dhidi ya Simba ambayo mwaka huo ilifika robo fainali ya klabu bingwa Afrika na kutolewa kwa mbinde na Nkana Red Devils (sasa Nkana FC) ya Zambia.

Licha ya njaa na shida kubwa ya safari yao, Milambo wakashinda 1-0 kwa bao la penalti la Said John.

Hakuna aliyeamini ushindi huu, hata wachezaji wenyewe wakishangaa sana, kasoro mganga.

Baada ya mechi, wakapata mgao wa shilingi 2 milioni na kugawana kila mchezaji shilingi elfu 80.

Ile bahati nasibu walioicheza ikawalipa. Hata hivyo, ili kupata kiasi hiki, ilibidi wachezaji wengine ambao hawakucheza, wakae magetini kulinda mapato.

Kumbuka walikuja wachezaji peke yao, bila kocha wala kiongozi yoyote, lakini wakarudi na alama 3 wakati ule ushindi ni alama mbili na sare ni alama moja.

Japo walikuja wenyewe, lakini taarifa zilipofika Tabora kwamba wachezaji walijisafirisha, na bahati nzuri wakavuna alama basi uongozi wa mkoa ukawakatia tiketi za treni daraja la pili kurudi Tabora.

Wakapokelewa kishujaa huku bendi ya Tabora Jazz ikitumbuiza kuanzia stesheni hadi klabuni.

Morali ikawa imerudi na hatimaye kushinda 1-0 mchezo wao wa mwisho dhidi ya RTC Kagera, na kunusurika kushuka.

Ni ile safari ya treni ndiyo iliwaokoa Milambo mwaka 1994, kama ambavyo ndugu zao Tabora United walivyookolewa na treni miaka 30 baadaye, yaani 2024.