Tshabalala aaga rasmi Simba, Yanga yatajwa
Muktasari:
- Tshabalala alijiunga na Simba mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar na amekuwa mmoja wa wachezaji waliodumu kwa muda mrefu katika kikosi hicho.
Dar es Salaam. Beki wa kushoto wa Simba SC, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ameaga rasmi klabu hiyo baada ya kuitumikia kwa zaidi ya miaka 11, akisema huu ni wakati wa kuangalia maendeleo yake binafsi.
Katika ujumbe wake wa kuaga aliouweka kwenye mitandao ya kijamii leo Jumamosi Julai 19, 2025, Tshabalala amesema kipindi alichokuwa ndani ya Simba kimejaa furaha, huzuni, shangwe na mafanikio, huku akisisitiza kuwa alitoa kila kitu kuiwakilisha klabu hiyo kwa heshima.
“Takribani miaka 11 ya furaha, huzuni, shangwe, vifijo, nderemo na masikitiko ndani ya mbuga,” ameandika Tshabalala.
“Kwa uaminifu mkubwa, weledi wa kiwango cha juu, kuvujwa jasho kuipigania nembo ya klabu, ndio ulikuwa msingi wa malengo yangu.”
Amesema uamuzi wake wa kuondoka umezingatia maslahi yake binafsi na ukuaji wake kitaaluma, huku akisisitiza kuwa ni maamuzi magumu lakini ya lazima kwa sasa.
“Nawashukuru viongozi, benchi la ufundi, wafanyakazi wote na mashabiki wa Simba kwa ushirikiano mkubwa mlionipa kwa kipindi chote nilichokuwa ndani ya klabu.”
Ameongeza kuwa, “Kipekee nawashukuru mashabiki kwa kuwa nami kipindi chote, kama mnavyonipenda na mimi nawapenda pia na nina imani mtaendelea kunipa mkono.”
Tshabalala alijiunga na Simba mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar na amekuwa mmoja wa wachezaji waliodumu kwa muda mrefu katika kikosi hicho huku akichangia mafanikio mbalimbali ikiwemo ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la FA na kushiriki michuano ya kimataifa.
Hadi sasa haijawekwa wazi kama beki huyo ataendelea kucheza soka au anajiandaa na maisha mengine nje ya uwanja, lakini taarifa zinaeleza kuwa bado ana ofa kutoka klabu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Pia, kuna tetesi huenda beki huyo akajiunga upande wa pili kwa watani wa Simba ambao ni Yanga.
Katika ujumbe wake, Tshabalala pia amemshukuru meneja wake Carlos Carlos kwa kusimama naye bega kwa bega katika kipindi chote cha utumishi wake ndani ya Simba.