Ubabe wa Bellingham ulivyoipa England jeuri kwa Mexico
Muktasari:
- Katika mechi iliyokuwa na kila aina ya drama, mabao matatu ya England yalitosha kuipeleka timu hiyo hatua inayofuata licha ya kumaliza sehemu kubwa ya kipindi cha pili ikiwa na wachezaji 10 uwanjani.
Timu ya taifa la England imetinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya wenyeji wenza Mexico katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa alfajiri ya leo, Jumatatu kwenye Uwanja wa Estadio Azteca, jijini Mexico.
Katika mechi iliyokuwa na kila aina ya drama, mabao matatu ya England yalitosha kuipeleka timu hiyo hatua inayofuata licha ya kumaliza sehemu kubwa ya kipindi cha pili ikiwa na wachezaji 10 uwanjani.
Mchezo ulianza kwa kuchelewa kwa saa moja kabla ya kuanza huku dakika za mwanzo zikishuhudia Mexico ikitawala kwa kushambulia kwa kasi kikubwa mbele ya mashabiki wake walioujaza Uwanja wa Azteca.
Mexico ilikaribia kufungua mabao mapema kupitia kwa mshambuliaji mkongwe Raúl Jiménez aliyepiga kichwa kizuri akiwa karibu na lango lakini kipa Jordan Pickford aliokoa na kuinyima Mexico bao la mapema.
England ilijibu mashambulizi yake kupitia Anthony Gordon aliyefanya kazi kubwa kuokoa mpira usitoke nje kabla ya kupiga shuti lililodhibitiwa vizuri na kipa Raúl Rangel.
Kadiri mchezo ulivyoendelea, England ilianza kutawala na dakika ya 36 ilivunja ukimya baada ya Bukayo Saka kupiga krosi iliyomkuta Jude Bellingham aliyeunganisha kwa kichwa na kuiandikia England bao la kwanza.
Dakika mbili baadaye, nyota huyo wa Real Madrid aliendeleza ubora wake kwa kufunga bao la pili baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa nahodha Harry Kane na kuupiga mpira wavuni kwa utulivu mkubwa, akifikisha mabao manne kwenye michuano hiyo.
Hata hivyo, Mexico haikukata tamaa. Dakika chache kabla ya mapumziko, Julián Quiñones aliifufua timu yake kwa kufunga bao kali lililompita Pickford na kupunguza tofauti ya mabao kuwa 2-1 huku mashabiki wa nyumbani wakirejea mchezoni.
Kabla ya mapumziko, Jiménez alikaribia kusawazisha kwa kichwa kingine lakini Pickford aliendelea kuwa shujaa kwa kuokoa mpira huo na kuutoa juu ya lango.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa kutoka pande zote mbili. England ilikaribia kuongeza bao kupitia Nico O'Reilly ambaye shuti lake lililoguswa kidogo liligonga mwamba.
Hata hivyo, mambo yalibadilika ghafla baada ya beki Jarell Quansah kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kufuatia marejeo ya VAR yaliyobaini alimchezea vibaya mpinzani wake.
Licha ya kupungua mchezaji mmoja, England haikuyumba. Dakika ya 60 Anthony Gordon aliangushwa ndani ya eneo la hatari na kipa Raúl Rangel, mwamuzi akaamuru penalti ambayo Harry Kane aliitumia vyema kufunga bao la tatu na kuipa England uongozi wa 3-1.
Mexico nayo ilipata penalti baada ya VAR kubaini Kane alimfanyia madhambi mchezaji wa Mexico ndani ya eneo la hatari. Jiménez hakufanya makosa alipofunga na kufanya matokeo kuwa 3-2, hali iliyorejesha matumaini kwa wenyeji.
Dakika za mwisho zilikuwa za presha kubwa huku Mexico ikisukuma mashambulizi mfululizo ikisaka bao la kusawazisha lakini safu ya ulinzi ya England iliyoongozwa na Pickford ilisimama imara hadi filimbi ya mwisho.
Ushindi huo unaifanya England kufuzu robo fainali ikiwa bado haijapoteza mchezo wowote katika mechi saba mfululizo kwenye michuano hiyo.
Katika hatua inayofuata, kikosi cha kocha Thomas Tuchel kitavaana na Norway katika robo fainali huku kikiendelea na ndoto ya kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966.
Kwa upande wa Mexico, kipigo hicho kimekatisha rekodi yao ya kutopoteza mechi 12 mfululizo na pia kuendeleza kusubiri kufika robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu walipoandaa mashindano hayo mwaka 1986.