Ukonga Stendi United yatinga nusu fainali Ng'ombe Cup

Dar es Salaam. Timu ya Ukonga Stendi United imeingia nusu fainali baada ya kuifunga kwa mikwaju ya penalti goli 5-4 dhidi ya timu ya Mbuyuni iliyopo Mongolandege.

Mkurugenzi wa timu hiyo ambaye ni mwenyekiti wa Serikali ya mtaa Mwembe Madafu, Mbaraka Mohamed akizungumza kwenye mashindano ya kombe la Ng'ombe Cup lililofanyika kwenye viwanja vya Cosovo Msimbazi, alisema  lengo lao kutangaza michezo kwenye Kata ya Ukonga.

"Lengo la michezo hii kuibua vipaji vya vijana na waachane na utumiaji wa madawa ya kulevya ikiwemo bangi na tunaomba wadau wa michezo wajitokeze kuisaidia timu ya Ukonga Stendi United kuchangia vifaa vikiwemo jezi, mipira na groves," alisema Mohamed.

Alisema kipindi cha Kwanza timu ya Ukonga Stendi United iliifunga timu ya Mbuyuni bao moja na ilipofika kipindi cha pili walisawazisha kwa mkwaju wa penalti.

Mohamed alisema dakika ziliongezwa hivyo timu ya Ukonga Stendi United iliifunga timu ya Mbuyuni Kwa mikwaju ya penalti tano kwa nne na kuwafanya waingie nusu fainali.

Hivyo timu hiyo itacheza nusu fainali  na timu ya Ulongoni A kwenye viwanja hivyo vya Cosovo Septemba 22 mwaka huu.

Naye Diwani wa Kata ya Ukonga ambaye alikuwa mgeni rasmi, Ramadhani Benders aliwataka vijana kuyatumia mashindano hayo kujipatia mazoezi ya mwili ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu.

Pia alisema mashindano hayo yataibua vipaji vya michezo ambavyo vitawasaidia kujipatia ajira mbali na mchezo huo kwenye Kata hiyo atajitahidi kuibua mchezo wa mpira wa miguu Kwa wanawake na mchezo wa kikapu

"Ninaamini katika kata yangu kuna vipaji vingi vinavyotakiwa kubuliwa," alisema Bendera