Uruguay yarejea kwa ndege za abiria baada ya kutolewa Kombe la Dunia
Muktasari:
- Uruguay ilitupwa nje ya mashindano hayo baada kuruhusu kipigo katika mchezo wa mwisho dhidi ya Hispania.
Baada ya Shirikisho la Soka la Uruguay (AUF) kufuta safari ya ndege maalumu iliyokuwa imepangwa kuwarejesha wachezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo kutoka kambini nchini Mexico kwenda Montevideo, timu hiyo imelazimika kutumia ndege za abiria za kawaida kufuatia kuondolewa katika hatua ya makundi ya Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Uruguay, wachezaji wamelazimika kutumia ndege za kawaida za abiria, huku wakisafiri katika makundi tofauti kulingana na ratiba za mashirika ya ndege.
Uruguay iliingia katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Hispania ambao ilihitajika kupata ushindi ili kufuzu hatua ya 32 bora, baada ya kutoka sare katika mechi zake mbili za awali dhidi ya Saudi Arabia na Cape Verde.
Hata hivyo, ndoto zao zilififia baada ya kufungwa ba 1-0 katika mchezo uliochezwa Guadalajara, Mexico. Bao pekee la mchezo lilitokana na kosa la kipa katika dakika ya 42, huku Uruguay ikishindwa kusawazisha hadi mwisho wa mchezo.
Kikosi cha timu ya taifa ya Uruguay baada ya kutua kwenye ardhi yao ya nyumbani. Picha na Mtandao
Matokeo hayo yaliiondoa Uruguay, taifa lenye historia kubwa katika soka la dunia.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Uruguay, Marcelo Bielsa, alionyesha masikitiko makubwa kuhusu safari yake ya miaka mitatu akiwa na timu hiyo.
"Sijaliachia soka la Uruguay chochote, kwa sababu kazi ya kocha hupimwa kwa matokeo. Nafasi ya nne katika kufuzu Kombe la Dunia, nafasi ya tatu Copa América na hata mashindano haya havina maana ikiwa hukufanikiwa kufikia malengo," amesema Bielsa.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 70 kutoka Argentina anatarajiwa kuondoka kwenye benchi la Uruguay, huku shirikisho la soka la nchi hiyo likianza mchakato wa kutafuta mrithi wake kuelekea maandalizi ya Kombe la Dunia 2030, ambalo Uruguay itakuwa miongoni mwa mataifa yatakayokuwa wenyeji wa mechi za maadhimisho ya miaka 100 tangu mashindano hayo yaanze mjini Montevideo mwaka 1930.